1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia: Al-Shabaab yakamata kambi ya jeshi ya Janay Abdale

Daniel Gakuba
7 Machi 2023

Duru rasmi kutoka maafisa wa Somalia zimearifu kuwa wapiganaji wa kundi la al-Shabaab wameikamata kambi ya jeshi iliyo katika jimbo la Jubbaland kusini mwa Somalia, ambayo walipokonywa na jeshi la serikali mwezi Januari.

https://p.dw.com/p/4OMZS
Somalia Kämpfer der al-Schabaab-Miliz
Picha: Mohamed DAHIR/AFP/Getty Images

Tangu mwaka jana, Kundi la Al-Shabab ambalo lina mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka jeshi la taifa linaloshirikiana na wanamgambo wa kiukoo.

Katika muda wa juma zima lililopita hakukuwepo mapigano yoyote, hali iliyowafanya wachambuzi kufikiria kwamba nguvu za serikali kuiandama al-Shabaab zimepungua.

Serikali ya Mogadishu ilijibu kuwa ilikuwa ikitumia mapumziko hayo kupanga mashambulizi makubwa zaidi.

Kambi iliyochukuliwa na Al-Shabab Jumanne ni ya Janay Abdale, ambayo iko umbali wa kilomita zipatazo sitini kutoka mji wa bandari wa Kismayu.