1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArmenia

Watu 85,000 wakimbilia Armenia kutoka Nagorno-Karabakh

Sylvia Mwehozi
29 Septemba 2023

Takribani watu elfu 85,000 wameomba hifadhi nchini Armenia baada ya Azerbaijan kuudhibiti mkoa unaozozaniwa wa Nagorno-Karabakh huku shirika la UNHCR likisema idadi yao inaweza kuongezeka.

https://p.dw.com/p/4Wx9Y
Armenien I Kornidzor, der ersten Anlaufstelle für geflüchtete aus Berg-Karabach
Picha: Alexander Patrin/TASS/picture alliance

Msemaji wa serikali ya Armenia Nazeli Baghdasaryan, amesema hii leo kwamba idadi hiyo ya watu ni wale waliolazimishwa kukimbia makaazi yao katika mkoa wa Nagorno-Karabakh. Kwa mujibu wa taarifa ambazo hazijathibitishwa, Waarmenia wapatao 120,000 hapo awali, walikuwa wakiishi katika mkoa wa Nagorno-Karabakh. Mnamo wiki hii, Azerbaijan inayoongozwa na utawala wa kiimla, kupitia mashambulizi yake ya kijeshi ilichukua udhibiti kamili wa mkoa huo ambao umezozaniwa kwa miongo kadhaa.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR limethibitisha taarifa za kukimbia kwa idadi hiyo ya watu likitaja idadi kubwa zaidi ya elfu 88,000 na kwamba idadi yao inaweza kuongezeka kufikia 120,000.

Jamhuri isiyotambulika ya Artsakh ambayo ilikuwa ikiongoza jimbo la Nagorno-Karabakh ilitangaza wiki hii kuwa itahitimisha uwepo wake kuanzia Januari Mosi mwaka ujao. Waermenia waliokuwa wakiishi katika mkoa huo, wamekuwa na hofu ya kuteswa na vurugu kutoka upande wa Azerbaijan. Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan anaishutumu jirani yake Azerbaijan kwa kampeni ya "safisha safisha ya kikabila".

Maelfu ya wakaazi wa Nagorno-Karabakh
Maelfu ya wakaazi wa Nagorno-Karabakh wakikimbilia ArmeniaPicha: Vasily Krestyaninov/AP/picture alliance

"Uhamaji wa Waarmenia kutoka Nagorno-Karabakh unaendelea kutokana na sera ya safisha safisha ya kikabila ya Azerbaijan. Uchambuzi unaonyesha kuwa katika siku zinazokuja hakutokuwa na raia hata mmoja wa Armenia atakayesalia Nagorno-Karabakh. Haya ni matokeo ya moja kwa moja ya kitendo cha safisha safisha ya kikabila na kuwaondoa watu katika nchi kama ambayo tumekuwa tukieleza jumuiya ya kimataifa kwa muda mrefu," amesema waziri mkuu Pashinyan.

Wakimbizi: Armenia yawapokea zaidi ya wakimbizi 50,000 kutoka Nagorno-Karabakh

Wakati hayo yakijiri, idadi ya vifo vilivyotokana na mlipuko katika ghala ya mafuta mkoani Nagorno-Karabakh imepanda na kufikia watu 170. Mlipuko huo ulitokea siku chache baada ya wapiganaji wanaotaka kujitenga katika mkoa huo kutangaza kwamba watasalimisha silaha na kujiunga upande wa Azerbaijan. Mamlaka zilisema awali kwamba mlipuko huo uliwaua watu 68 na kuwajeruhi wengine 200. Mlipuko huo ulitokea wakati wakimbizi walipokuwa wakijaza mafuta kwa ajili ya safari ya kukimbilia Armenia.

Soma pia: Azerbaijan yasema zaidi ya wanajeshi wake 100 wamekufa kwenye operesheni ya kuwania Nagorno Karabakh

Katika hatua nyingine wajumbe kutoka wizara za ulinzi za Azerbaijan na Armenia, wamewasili katika mji wa Urusi wa Tula kwa ajili ya mkutano wa baraza la mawaziri wa ulinzi wa nchi za Jumuiya ya Mataifa Huru CIS. Shirika la habari la Urusi, TASS limeripoti kwamba wajumbe kutoka nchi za Urusi, Azerbaijan, Armenia, Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan watashiriki mkutano huo. Mkutano huo utajadili masuala kadhaa haswa juu ya ushirikiano wa kijeshi na hali ya sasa katika nyanja ya siasa za ulimwengu.

Vyanzo: reuters/dpa/afp