1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Watoto 300 wahamishiwa mahala salama, Sudan

Lilian Mtono
8 Juni 2023

Karibu watoto 300 wamehamishwa katika kituo cha kulelea yatima kilichopo Khartoum. Maafisa wa huduma za misaada wamesema watoto hao walikwama kituoni hapo wakati mapigano makali yalipokuwa yakiendelea kote mjini humo.

https://p.dw.com/p/4SKji
UNICEF imefanikiwa kuwahamisha watoto 300 wa Sudan na kuwapeleka mahala salama ili kuwaepusha na athari za mapigano.
Shirika la kuhudumi watoto la Umja wa Mataifa, UNICEF limesema watoto nchini Sudan wanakabiliwa na hali ngumu kutokana na mapigano yanayoendelea.Picha: Denis Balibouse/REUTERS

Maafisa hao walifanikiwa kuwaokoa watoto hao baada ya wenzao karibu 71 kufariki kutokana na njaa ama magonjwa, tangu katikati ya mwezi Aprili.

Janga hilo lililotokea kwenye kituo cha yatima cha Al-Maycoma liligonga vichwa vya habari mwishoni mwa mwezi uliopita wakati mapigano yalikuwa yamepamba moto kote mjini Khartoum kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha Dharura cha RSF.

Vifo hivyo aidha vimeashiria mashaka makubwa yanayowakabili raia tangu mapigano hayo yalipoanza katikati ya mwezi Aprili.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Ricardo Pires, ameliambia shirika la habari la AP kupitia barua pepe kwamba, karibu watoto 300 waliokuwa kwenye kituo hicho cha Al-Mayqoma wamehamishiwa katika eneo salama, huko kaskazinimashariki mwa taifa hilo.

Gari lililowabeba misaada ya kiutu kutoka shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF likiwa limesimama mbele ya nyumba ya kulelea watoto
Picha: Nazim Sirag/AP/picture alliance

Pires amesema, kwa sasa wizara za maendeleo ya jamii na afya za nchini Sudan, ndizo zinawazohudumia watoto hao na UNICEF litakuwa linatoa misaada ya kiutu ambayo ni pamoja na za tiba, chakula, elimu na michezo. Amesema watoto hao tayari wamefanyiwa uchunguzi wa kiafya baada ya safari ndefu kutokea Khartoum hadi kwenye makazi hayo mapya na kuongeza kuwa kila mtoto atakayetakiwa kulazwa, atapewa huduma hiyo.

Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu lililosaidia kuwahamisha watoto hao limesema watoto wa kati ya mwezi mmoja hadi miaka 15 walihamishwa baada ya kufunguliwa kwa njia salama hadi mji wa Madani, ambao ni mkubwa katika mkoa wa Jazira, uliopo umbali wa maili 85 kutoka Khartoum.

Mkuu wa shirika hilo nchini Sudan Jean-Christophe Sandoz amesema ni furaha kwao kuona hatimaye watoto hao wako kwenye mikono salama, baada ya kukwama kituoni hapo kwa wiki sita, huku mapigano makali yakiendelea mjini Khartoum.

Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema watoto hao wako salama kwa sasa na wanahudumiwa na wizara za maendeleo ya jamii na afya za Sudan.
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Vojinovic

"Ilikuwa inaumiza sana kuwaona hawa watoto ambao miongoni mwao wana matatizo ya akili na mengine ya kiafya wakikwama kituoni kwa wiki sita kwa sababu ya mapigano. Lakini tumefarijika sana kwamba tumeweza kuwaleta mahala salama sasa na wanaweza kupata huduma muuafaka za afya," alisema mkuu huyo wa UNICEF.

Mzozo nchini Sudan umesababisha zaidi ya watu milioni 1.9 kukimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na karibu 477,000 waliokinbilia mataifa jirani, hii ikiwa ni kulingana na shirika la wahamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM. Raia wengine bado wamekwama majumbani kwao, wakiwa wanaogopa kutoka nje, ilihali wakikabiliwa na uhaba wa chakula na maji.

Soma Zaidi: UNHCR:Takriban watu 200,000 kutoka Sudan wamekimbilia nchi jirani

Kulingana na msemaji wa katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric tangu Mei 24, ofisi ya umoja huo inayoratibu huduma za kiutu imefanikiwa kupeleka tani karibu 7,400 za misaada katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Soma Zaidi: Mataifa zaidi kuwaondoa raia wao Sudan