1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani DRC wafanya mazungumzo Afrika Kusini

Iddi Ssessanga
14 Novemba 2023

Wajumbe wa viongozi wa juu wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wako nchini Afrika Kusini kujadili uratibu wao kuelekea uchaguzi mkuu ujao katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/4YnXA
Wagombea urais wa DR Kongo, Felix Tshisekedi Moise Katumbi Denis Mukwege na Martin Fayulu.
Baadhi ya wagombea urais wa DR Kongo, Felix Tshisekedi Moise Katumbi Denis Mukwege na Martin Fayulu.Picha: AFP/Getty Images, picture alliance, G. Kusema, DW

Wachambuzi wengi wanamwona Rais Felix Tshisekedi kuwa na uwezekano wa kushinda kura hiyo, ikizingatiwa kwamba upinzani wa kisiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umegawanyika kati ya wapinzani kadhaa.

Siku ya Jumatatu, wajumbe wanaowakilisha wanasiasa watano wakuu wa upinzani -- ambao wote wanashiriki uchaguzi ujao -- walifika katika mji mkuu wa utawala wa Afrika Kusini Pretoria kwa mazungumzo.

Walihusisha wajumbe wa Moise Katumbi, mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa jimbo la Katanga; mgombea urais wa zamani Martin Fayulu; waziri mkuu wa zamani Augustine Matata Ponyo; Delly Sesanga, mbunge; na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel 2018 Denis Mukwege.

Soma pia: Wagombea 26 kuwania kiti cha urais Kongo

"Ugombea wa pamoja utahitajika ili kuepuka kutawanya kura za upinzani," alisema mshiriki mmoja wa mazungumzo hayo ambaye alikataa kutajwa jina.

Lakini mshiriki mwingine, ambaye pia aliomba kutotajwa jina, alisema mazungumzo hayo yalilenga kutafuta "utaratibu wa pamoja wa kuepusha udanganyifu” katika uchaguzi huo.

Felix Tshisekedi Präsident DR Kongo
Rais wa DRC Felix Tshisekedi anawania muhula wa pili akichuana na wagombea wengine kadhaa, katika uchaguzi mkuu wa Desemba 20.Picha: Isa Terli /AA/picture alliance

"Hatukwepeki mjadala wa mgombea mmoja, lakini tunachohitaji zaidi ya yote ni ukweli kwenye sanduku la kura," alisema.

Mazungumzo hayo mjini Pretoria yanaweza kudumu hadi Alhamisi, na yameandaliwa chini ya uangalizi wa shirika lisilo la kiserikali la Afrika Kusini la "In Transformation Initiative," ITI.

Soma pia: Congo kulegeza baadhi ya masharti ya utawala wa kijeshi

"Wanataka kuanza mchakato wa kuzungumza na kuona jinsi gani wanaweza kushirikiana," Ivor Jenkins, mkurugenzi mkuu wa ITI alisema. "Lengo kuu ni jinsi gani DRC inaweza kuwa demokrasia yenye nguvu, na mazingira ya vyama vingi, kuwa na uchaguzi huru na wa haki."

Wagombea 26 kwa jumla wanawania uchaguzi wa rais wa DRC, ambao unafanyika wakati mmoja na kura za wabunge, majimbo na manispaa. Kati ya wagombea waliokutana Pretoria, Katumbi, Fayulu, Ponyo na Sesanga, ni wanasiasa wenye uzoefu.

Denis Mukwege, daktari wa upasuaji wa magonjwa ya wanawake ambaye alishinda Tuzo ya Nobel kwa juhudi zake za kukomesha unyanyasaji wa kijinsia, na asiye na uzoefu rasmi wa kisiasa, alitangaza kugombea kwake Oktoba.

Chanzo: AFPE