1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 wauzingira mji wa Sake, DRC

13 Februari 2024

Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limetumia ndege za kivita kuwarudisha nyuma waasi wa M23 waliokuwa wameuzingira mji wa Sake uliopo kilometa 27 magharibi mwa mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini.

https://p.dw.com/p/4cLK4
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Muasi wa M23
Waasi wa M23 huko Kibumba, Jamhuri ya Kidemokrasi ya KongoPicha: GLODY MURHABAZI/AFP via Getty Images

Taarifa zinasema kuwa watu wasiopungua 7 walijeruhiwa  ndani ya kambi moja ya wakimbizi katikati mwa mji huo ambako hali ya wasiwasi ilitanda hadi Jumatatu jioni.

Mamia ya Watu  waliokuwa wameanza kurudi majumbani mwao mwishoni mwa wiki iliyopita waliuacha tena mji huo wa Sake baada ya wapiganaji wa M23 kuuzingira.

Vyanzo vya ndani vimeeleza kuwa kundi hilo linalodaiwa kupata usaidizi wa jeshi la Rwanda lilizidisha mashambulizi yake kwenye vijiji vya Kihuli, Kimoka na Luhonga kilometa karibu 5 na mji huo ambako milio ya silaha nzito iliendelea kusikika hadi jana jioni.

M23 yavidhibiti baadhi ya vijiji

Ikiwa wengi wa raia walikuwa wakikimbia nyumba zao, wengine walikuwa wakiyashambulia magari ya walinda amani wa umoja wa mataifa, MONUSCO wakiwashutumu kuwasaidia M23 kama anavyoeleza raia huyu wa Sake.

DR Kongo Muasi wa M23
Mpiganaji wa waasi wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya KongoPicha: GLODY MURHABAZI/AFP via Getty Images

"Ni takribani kilometa 5 kutoka mji wa sake ndipo mapigano yaliendelea na hadi wakati huu. Vita hivi vya M23 vimesababisha maafa mengi kwa raia ikiwemo hata vifo. Kwa hiyo wananchi mjini sake walishutumu pia kikosi cha Monusco kufanya kazi na waasi wa M23  na hiyo ikapelekea risasi kurindima nakuongeza hofu kwa wananchi walio anza kukimbia ," alisema mkaazi huyo wa Sake.

Hadi mchana wa Jumanne, kundi hilo lililopiga hatua kwa kuvidhibiti baadhi ya vijiji wilayani Masisi, limeendelea kukita kambi kando na mji huo na kuzifunga barabara zote za kusambaza bidhaa hadi mji mkuu wa jimbo, Goma. Pascal Kulimushi ni mwakilishi wa bunge la vijana mjini Sake ambaye hivi sasa yuko mafichoni.

"Muda huu waasi wa M23 wanadhibiti mji mdogo wa Lutobogo, Ngumba na mlima wa Karongora kilometa 3 na mji wa sake. Ni kweli kwamba waasi wameuzingira mji huo wa sake lakini bado jeshi la kongo lapatikana katika mji huo," alisema Kulimushi.

Mapigano yaelekea mji wa Goma

Akizungumza na wananchi wa Sake mwanzoni mwa juma hili,Peter Chirimwami, gavana wa jijeshi mkoani Kivu Kaskazini alisema,

"Ikiwapo nimewasili hapa ni kwa ajili ya kuwatolea pole, juweni kwamba raisi anawawekea matumaini kuhusu Mnusco inabidi kuwa watulivu sababu mkiwashambulia mtampatia adui ushindi. Kamwe hatuta kubali mufanye fujo dhidi ya Monusco," alisema Chirimwami.

Mapigano hayo yanayoanza kuukaribia mji wa Goma yamesababisha watu zaidi ya milioni saba kuwa wakimbizi baadhi ikiwa ni wale kutoka wilayani Masisi na Rutshuru wanaohangaika sasa kwenye kambi za wakimbizi. 

DR Kongo Weiterhin Kämpfe im Osten | Rusayo IDP Camp
Msichana na mvulana wakibeba mtungi wa maji kambi ya Rusayo, karibu na GomaPicha: Alexis Huguet/AFP

Ripoti mpya  ya Umoja wa Mataifa, imeonesha kuwa jeshi la Rwanda linalounga mkono waasi wa M23 linatumia silaha  zenye uwezo wa juu kama vile makombora ya kutoka ardhini kwa kuzidungua ndege za kivita, vifaa vinavyoweza kuwapa uwezo wa kusonga mbele katika vita mashariki mwa Kongo.