1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAfrika

Viongozi wa Afrika wataka ufadhili zaidi wa mataifa tajiri

Shisia Wasilwa
29 Aprili 2024

Viongozi wa Afrika wanayataka mataifa tajiri kujitolea kuchangia mfuko wa Benki ya Dunia kwa ustawi wa mataifa yanayoendelea na kuyawezesha kukabiliana na jinamizi la mabadiliko ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/4fJVe
Mkutao wa IDA, 2024| Kenya| Nairobi
Viongozi wa mataifa ya Afrika wakiwa mjini Nairobi kwa mkutano wa kilele wa IDA.Picha: Shisia Wasilwa/DW

Kwenye Kongamano la Maendeleo ya Kimataifa IDA linaloendelea jijini Nairobi nchini Kenya viongozi hao wamesema ili kufanikisha malengo hayo pana haja ya kufanywa mageuzi kwenye asasi za kimataifa ambazo hufadhili mataifa yanayostawi.

Rais William Ruto wa Kenya aliyefungua rasmi Kongamano hilo la siku mbili, alitangulia kwa kupaza sauti kwa  mashirika wafadhili kuitikia mchango wa Chama Cha Maendeleo ya Kimataifa-IDA.

Aidha alielezea kuwa mataifa ya Afrika yanakabiliwa na madeni yanayotishia kusambaratisha chumi zao. Chama cha Maendeleo ya Kimataifa-IDA ni Taasisi ya Benki ya Dunia ambayo hutoa mikopo kwa riba nafuu na za muda mrefu kwa mataifa yanayoendelea.

“Kuwekeza kiwango kikubwa cha fedha kwa IDA ni muhimu. Kikundi cha wataalamu huru wa mataifa ya G20 wanapendekeza kuongezwa mara tatu kwa fedha zinazotolewa kwa IDA kufikia dola bilioni 279 ifikapo mwaka 2030. Tusipuuze ushauri wa wataalam hao,” amesema Rais Ruto.

Mkutano wa IDA, 2024| Kenya| Nairobi
Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda akihutubia mkutano wa kilele wa IDA mjini Nairobi.Picha: Shisia Wasilwa/DW

Matamshi ya Rais Ruto yanajiri huku Mataifa ya Jumuiya ya Afrika yakikabiliwa na mafuriko mabaya kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mataifa husika.

Nchini Kenya pekee idadi ya maafa imefikia 100 huku watu waliopoteza makazi wakifikia watu elfu sitini. Hali ambayo wataalam wanasema imechangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Iwapo wafadhili wataahidi kutoa kiwango kidogo cha fedha kama viongozi wa Afrika wanavyopendekeza kiwango hicho kitaongezeka maradufu, kwani mwaka 2021 fedha hizo zilifikia dola bilioni 93.

Benki ya Dunia yaahidi kulegeza masharti ya kutoa mikopo 

Rais wa Benki ya Dunia Ajay Banga, ameahidi kupunguza mzigo wa masharti yanayotumika wakati wa kutoa mikopo kwa mataifa.

IDA 2024|Kenya|Nairobi
Viongozi na wawakilishi wa mataifa ya Afrika kwenye mkutano wa kilele wa IDA mjini Nairobi, Kenya.Picha: Shisia Wasilwa/DW

Amesema hatua hiyo itachochea mchakato wa kukopa kwa kasi kwa upande wa mataifa yanayokopa. Fedha hizo hutumiwa na serikali za mataifa yanayoendelea kuimarisha sekta za nishati, afya, kilimo na pia kujenga miundo msingi.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu ni mmoja wa viongozi 14 wa Afrika waliohudhuria kongamano hili. Yeye kwa upande wake amesema, “Tunaamini kuwa IDA 21, inastahili kuangazia zaidi mikopo yenye masharti nafuu itakayolipwa kwa miaka 50. Mikopo hiyo itasaidia kwa maendeleo ya mataifa ya Afrika."

Kikundi cha wataalamu huru wa mataifa ya G20 wanapendekeza kuongezwa mara tatu kwa fedha zinazotolewa kwa chama cha IDA kufikia dola bilioni 279 ifikapo mwaka 2030.

Viongozi hawa pia wamependekeza kutumia uanachama wa Umoja wa Afrika kushinikiza mataifa ya G-20 kuipa kipaumbele suala IDA kwenye mikutano yao yote.

IDA ina miradi 75 kote barani Afrika. Chama cha Maendeleo ya Kimataifa –IDA kilianzishwa mwaka 1960 kwa lengo la kupunguza umasikini kwa kutoa mikopo bila riba kwa miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha uchumi, ukuaji, usawa na kuinua hali ya wananchi.