1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vinicius aizamisha Barcelona

15 Januari 2024

Winga wa Real Madrid Vinicius Junior aliisaidia Real Madrid kupata ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya Barcelona katika fainali ya kombe la Super Cup iliyochezwa hapo Jumapili huko Riyadh Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/4bGQi
 Vinicius Junior
Winga wa Real Madrid Vinicius JuniorPicha: AP/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Vinicius alifunga magoli matatu katika kipindi cha kwanza cha mechi na akasherehekea magoli yake kwa mtindo anaoutumia mchezaji wa zamani wa Madrid Cristiano Ronaldo kila anapofunga.

"Nilisherehekea mabao yangu namna ile kwa ajili ya Cristiano Ronaldo kwasababu ni mchezaji ninayempenda mno na sasa hivi anacheza hapa Saudi Arabia. Kuhusu mechi, nina furaha sana kwa ajili ya timu yangu na kile tulichokifanya leo. Kucheza dhidi ya barcelona si rahisi na ni vigumu kuwafunga 4-1. Mechi ilikuwa nzuri ila nahisi tungelizuia lile goli la Lewandowski," alisema Vinicius.

Kwa upande wake kocha wa Barcelona Xavi Hernandez amewashambulia wachezaji wake kwa kusema huu ndio mchezo mbaya zaidi waliowahi kuuonyesha hadi pale msimu ulipofikia.

"Tumecheza vizuri hadi Lewandowski alipofunga ila hilo halikutosha. Tunastahili kujikosoa sana, tunastahili kuboresha viwango vyetu iwapo tunataka kushindana msimu huu kwa kweli. Tulifurahia na tulikuwa na matumaini ila hiyo haitoshi. Nataka kuwaomba radhi mashabiki wetu kwasababu hii siyo picha ambayo Barcelona inataka kuonyesha, hasa katika fainali dhidi ya Real Madrid," alisema Xavi.

Chanzo: Reuters/AP/AFP