1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana washiriki maadamano siku ya mazingira duniani

Ibrahim Swaibu
25 Septemba 2020

Maelfu ya vijana duniani, wakioongozwa na mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg wamefanya maandamano ya kutaka kuongezwa kwa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/3j14t
Fridays For Future | Berlin
Picha: Hannibal Hanschke/Reuters

Mwanaharakati wa mazingira  Greta Thunberg alijiunga na waandamanaji wengine, nje ya bunge la Sweden huku waandamanaji hao wakiweka umbali kati yao,  kuanzisha tena siku ya maandamano ya mazingira duniani ambayo ni ya kwanza kufanyika tangu ulimwengu kukumbwa na janga la virusi vya Corona.

Maandamano hayo yanalenga kuwataka wabunge kuheshimu Mkataba wa Mazingira wa Paris ambao unazitaka nchi zote tajiri na maskini kuongeza juhudi katika kupunguza kuongezeka kwa hali ya ujoto duniani.

Msichana  huyo  mwenye  umri  wa  miaka  17  amewambia waandishi  habari  kuwa  matumaini  makubwa ni kuweza kuuelimisha umma kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kushawishi maoni ya umma ili jamii iweze kuchukua tahadhari.

Maandamano kama hayo pia yamefanyika katika zaidi ya maeneo 3,100  duniani  na vijana kuungana na Thunberg chini ya vugugu lake maarufu kama ''Ijumaa  kwa  ajili  ya  mustakabali'' kuwataka watunga sera kuongeza juhudi katika kukabiliana na kupunguza athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Waandamanaji katika mataifa  ya Australia, Japan na Fiji  ndio waliokuwa wa kwanza kufanya maandamano hayo. Hata hivyo kutokana na janga la Covid 19, idadi ya walioshiriki imepunguzwa na wengi  wao kushiriki kupitia njia ya mtandao.

Nchini Australia maelfu ya wanafunzi walishiriki katika maandamano ya makundi ya watu 500 huku wengine wakishiriki kupitia mitandao ya kijamii kudai uwekezaji zaidi katika nishati jadidifu na kupinga ufadhili kwa miradi ya gesi. Waandalizi waliwaomba washiriki kuweka picha kwenye mitando ya kijamii na pia kushiriki katika mkutano wa mtandoani ambao umedumu kwa saa 24, wakati wale walioshuka mitaani wakitakiwa kuweka umbali kati yao.

Nako nchini Ufilipino, mwanaharaki wa mazingira Mitzi Jonelle Tan, mwenye umri wa miaka 22 ameikosoa serikali kwa kile alichosema ''kushindwa kuwalinda raia wake dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na zile za janga la Covid-19''

Katika wakati ambapo dunia inakabiliwa na majanga yatokanayo na mabadliko ya tabianchi ikiwemo moto mkubwa nchini Marekani na mataifa ya magharibi, kuongezeka kwa joto kali katika eneo baridi sana la aktiki ya Siberia pamoja na mafuriko nchini China, waandamanaji hao wanasema hatua yao ni kuwakumbusha wanasiasa kuwa  wakati dunia imeelekeza juhudi katika kukabiliana na janga la Covid-19, janga la mabadiliko ya tabia nchi  bado halijaisha.

Maandamano ya leo pia yanalenga kuonyesha mshikamano na watu, maeneo pamoja na jamii ambazo licha ya kutohusika katika uchafuzi mkubwa wa mazingira, ndio wahanga wakuu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi kama mafuriko kuongezeka kwa joto  pamoja na uvamizi wa nzige.

Vyanzo: AP/Reuters