1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine, Urusi zadai kudunguliana ndege zisizotumia rubani

Iddi Ssessanga
22 Desemba 2023

Urusi na Ukraine zimedai kila mmoja kudungua droni za mwenzake Ijumaa, Ukraine ikidai kudungua droni 24 kati ya 28 zilizorusha kuelekea Kyiv usiku, na Urusi ikisema mifumo yake imedungua droni 10 za Ukraine mjini Moscow.

https://p.dw.com/p/4aVoo
Ukraine | Mashambulizi dhidi ya Odessa
Mashambulizi ya droni katika mkoa wa Odesa, kusini mwa Ukraine.Picha: Nina Liashonok/Avalon/Photoshot/picture alliance

Urusi ilisema Ijumaa kuwa imedungua droni 10 za Ukraine juu ya anga ya Moscow na mikoa kadhaa ya mpakani, huku Kyiv ikiapa kuongeza uzalishaji wa droni katika miezi ijayo.

Mashambulizi ya droni katika ardhi ya Urusi yalikuwa nadra mwanzoni mwa mzozo wa Ukraine lakini yamekuwa yakiongezeka katika kipindi cha mwaka uliyopita, ikiwemo katika mji mkuu wa Urusi Moscow.

"Mifumo ya ulinzi wa anga katika wilaya ya mjini ya Podolsk ilizuwia shambulizi la droni iliyokuwa inaelekea Moscow," meya wa mji huo mkuu Sergei Sobyanin alisema.

Hakuna uharibifu au vifo vilivyoripotiwa ambako mabaki ya ndege hizo yalianguka na idara ya huduma za dharura ilikuwa inafanya kazi katika eneo la tukio, aliongeza Sobyanin.

Awali vikosi vya jeshi vilsiema vilizuwia mawimbi kadhaa ya mashambulizi na kuharibu droni tano katika mkoa wa mpakani wa Bryansk. Droni nyingine nne ziliharibiwa katika mkoa wa Kaluga, uliyopo karibu na Moscow, vilisema vikosi vya jeshi.

Ukraine yadai kudungua droni 24 kati ya 28 za Urusi

Kwa upande wake Ukraine ilisema ilidungua droni 24 kati ya 28 aina ya Shahed zilirushwa na Urusi katika shambulizi la usiku lililoharibu majengo ya makazi mjini Kyiv na ghala la nafaka katika mikoa ya kusini, maafisa walisema.

Soma pia: Umoja wa Ulaya washindwa kupata makubaliano kuisidia Ukraine

Walisema zaidi dazeni mbili za droni za Urusi ziliulenga mji mkuu, na kushambulia maghorofa ya 24, 25 na 26 ya jengo la makazi na kuwajeruhiwa watu wawili, na kusababisha uharibifu mdogo kwenye majengo mengine kadhaa ya makazi.

Ukraine, Odessa | shambulizi a droni la Urusi.
Askari wa zimamoto wakizima moto uliosababishwa na shambulizi la droni ya Urusi mjini Odessa.Picha: State Emergency Service of Ukraine in Odesa region/Handout/REUTERS

Katika eneo la kusini, Urusi ilijaribu tena kushambulia miundombinu ya bandari - shabaha ya mara kwa mara tangu ilipojitoa kwenye makubaliano yalioratibiwa na Umoja wa Mataifa yaliofikiwa baada ya uvamizi wa Februari 2022, ambayo yaliruhusu usafirishaji salaama wa nafaza za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi.

"...Mabaki ya droni iliyodunguliwa yaliharibu ghala. Kulikuwa na moto ambao ulidhibitiwa haraka na wafanyikazi wa kampuni," kamanda wa kijeshi wa kusini alisema kwenye jukwaa la ujumbe la Telegraph, akielezea shambulio katika mkoa wa Odesa.

Katika mkoa jirani wa Mykolaiv, kituo cha miundombinu kisichojulikana kilipigwa, na kusababisha moto, jeshi liliongeza. Hakukuwa na ripoti za majeruhi katika mikoa yote.

Baadaye siku ya Ijumaa, Mykola Oleschuk, mkuu wa kikosi cha anga cha jeshi la Ukraine, alisema kikosi hicho kimeangusha ndege tatu za kivita za Urusi SU-34 "katika upande wa kusini", ambao hakuutaja. Hata hivyo ripoti hiyo haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Marekani kuzilenga benki zinazosaidia vita vya Urusi nchini Ukraine

Marekani ilisema Ijumaa kuwa itaziwekea vikwazo benki za kigeni zinazounga mkono vita vya Urusi nchini Ukraine, katika jitihada mpya za kuweka shinikizo la kiuchumi kwa Moscow waakti ikibadili mtazamo kutoka mataifa ya magharibu kuelekea China.

Chini ya amri ya rais itakayotiwa saini Ijumaa na Rais Joe Biden, Marekani itaweka kile kinachoitwa vikwazo vya pili dhidi ya taasisi za fedha zinazoyafadhili makampuni ambayo tayari yamewekewa vikazo kwa kuisadia sekta ya ulinzi ya Urusi.

Urusi tayari imepoteza zaidi ya zana 13,000 za kivita, ikiwemo vifatu, droni na mifumo ya makombora, kulingana na tathmini ya Marekani.

Soma pia: Zelensky awashawishi Wamarekani kuendelea kuisaidia Ukraine

"Tunatuma ujumbe usio na shaka: mtu yeyote anayeunga mkono juhudi haramu za vita vya Urusi yuko hatarini kupoteza ufikiaji wa mfumo wa kifedha wa Marekani," Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa kitaifa wa Biden, alisema katika taarifa.

Sullivan alisema vikwazo hivyo vipya "vitaendelea kuimarisha skrubu kwenye mashine ya vita ya Urusi na wawezeshaji wake," akiongeza kuwa hatua za awali "zimelishusha hadhi" jeshi la Urusi, ambalo kwa muda mrefu lilionekana kuwa miongoni mwa vikosi vya kutisha zaidi duniani na ambalo katika miezi ya hivi karibuni limekuwa likitegemea manunuzi ya silaha kutoka mataifa yaliowekewa vikwazo ya Korea Kaskazini na Iran.

Washington Marekani| Bidenna Zelenskiy
Rais wa Marekani Joe Biden akisaliamiana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy mjini Washington Desemba 12, 2023. Biden amesaini amri ya vikwazo dhidi ya taasisi za fedha zinazowezesha sekta ya ulinzi ya Urusi.Picha: Yuri Gripas/UPI Photo/IMAGO

Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen alisema katika taarifa kwamba wanategemea taasisi za fedha zitafanya kila juhudi kuhakikisha haziiwezeshi Urusi ama kwa kujua au kutojua, kukwepa vikwazo, na kuongeza kuwa hawatasita kutumia zana mpya zitakazotolewa na mamlaka kuchukua hatua kali dhidi ya taasisi zinazowezesha vita vya Urusi.

Lakini Urusi tangu kuanza kwa vita imekuwa ikifanya kazi kwa kasi kupunguza utegemezi wake kwa nchi za Magharibi, ikijitenga na biashara ya dola, euro, sterling na yen. Wakati huo huo benki kubwa zaidi za China zimeongeza mkopo wa mabilioni ya dola kwa Urusi kwa sarafu yake ya renminbi tangu vita huku taasisi za Magharibi zikiondoka.

Uholanzi kuanza kutoa ndege za F-16 kwa Ukraine

Serikali ya Uholanzi ilitangaza Ijumaa kuwa inajiandaa kutoa ndege 18 za kivita za F-16 kwa Ukraine, katika hatau inayoliongezea nguvu jeshi la taifa hilo linalokabiliwa na vita, ambalo linazidi kuwa na wasiwasi kuhusu msaada kutoka kwa washirika wake wa Magharibi.

Waziri wa ulinzi wa Uholanzi, Kajsa Ollongren, alituma barua kwa bunge akibainisha mpango wa kuchangia ndege za kisasa ambazo zilizinduliwa kwa mara ya kwanza katika majira ya joto. Uamuzi huo wa Ijumaa ni hatua muhimu kuelekea kupeleka ndege katika anga ya Ukraine, lakini hakusema ni lini zitawasilishwa.

Serikali ilisema hatua hiyo "inaruhusu wafanyakazi na bajeti kutengwa kuandaa vifaa" vitakavyotumwa Ukraine.

"Kwa F-16, Ukraine inaweza kujilinda vyema dhidi ya mashambulizi ya Urusi," Ollongren alisema katika taarifa.

Aliongeza kuwa ndege hizo "ni muhimu sana kwa sababu uvamizi unaoendelea wa Urusi hauonyeshi dalili ya kuisha. Ndiyo maana tunaendelea bila kusita na uungaji mkono wetu kwa Ukraine."

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alitembelea kambi ya jeshi la anga katika mji wa kusini mwa Uholanzi wa Eindhoven mwezi Agosti kukagua ndege mbili kati ya hizo, siku ambayo Uholanzi na Denmark zilisema zingetoa msaada wa ndege ili kuimarisha juhudi za vita vya Ukraine.

Ndege ya kivita ya kisasa chapa F-16.
Ndege ya kisasa ya kivita chapa F-16.Picha: Ssgt. Samuel Earick/U.S Air/Planet Pix via ZUMA Press/picture alliance

Mwezi uliopita, Romania ilizindua kituo cha mafunzo cha kimataifa kwa marubani wa ndege za F-16 kutoka nchi washirika na washirika wengine, ikiwa ni pamoja na Ukraine.

Soma pia: Uholanzi na Denmark kuipatia Ukraine ndege za kivita F-16

Kituo cha mafunzo katika kambi ya jeshi la anga kusini-mashariki mwa Romania kitalenga kuongeza ushirikiano kati ya washirika wa NATO, na kuweka vyema muungano wa kijeshi "kukabiliana na changamoto ngumu" katika eneo la Ulaya Mashariki na eneo la Bahari Nyeusi, wizara ya ulinzi ya Romania ilisema.

Romania ilisema wakati huo kwamba ndege hizo za kivita zenye nguvu zilizotengenezwa na Marekani zitatolewa na jeshi la anga la Uholanzi huku kampuni ya kutengeneza ndege ya Lockheed Martin ikitoa wakufunzi na matengenezo katika kituo cha mafunzo.

Serikali ya Uholanzi ilisema Ijumaa bado inapaswa kuamua ikiwa itatoa kibali cha usafirishaji wa ndege hizo "ili kuzuia matumizi yasiyofaa." Wizara ya mambo ya nje itafanya tathmini hiyo kwa kuzingatia sheria za usafirishaji wa silaha za Umoja wa Ulaya.

Denmark, Norway na Ubelgiji, pia zimetangaza kuipa Ukraine ndege kama hizo, baada ya Marekani kuidhinisha utumaji wake kupambana dhidi ya Urusi, mara baada ya kukamilika kwa mafunzo ya marubani.

Stoltenberg: Urusi imeipoteza Ukraine milele

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihani NATO, Jens Stoltenberg, amesema anaamini Urusi imeipoteza Ukraine milele kutokana na vita hivyo, na kwamba haitoweza kutimiza lengo lake licha ya juhudi kubw aza kijeshi tangu uvamizi wa Februari mwaka jana.

"Madhumuni yote ya uvamizi huu ilikuwa kuizuia Ukraine kuelekea NATO na Umoja wa Ulaya. Ukraine sasa iko karibu na NATO na Umoja wa Ulaya kuliko hapo awali," aliiambia dpa katika mahojiano muda mfupi kabla ya Krismasi. "Huku ni kushindwa kwa kimkakati kwa Urusi."

"Rais Putin ameipoteza Ukraine milele," Stoltenberg alisema, akimaanisha ukweli kwamba Urusi iliiona Ukraine kama sehemu ya himaya yake ya ushawishi kwa miongo kadhaa.

Ubelgiji | NATO | Mkutano kati ya Stoltenberg na Zelenskiy.
Rais Zelenskiy akiwa na katibu mkuu wa NATO stoltenberg.Picha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Waziri mkuu huyo wa zamani wa Norway ana uhakika kwamba Ukraine hatimaye itafikia lengo lake la kujiunga na NATO. Pia alisema kuwa Urusi ilikuwa ikilipa gharama kubwa sana kwa vita vyake. "Urusi imepoteza mamia ya ndege, maelfu ya vifaru vya kivita, na vifo au majeruhi 300,000. Uchumi wao ni dhaifu. Wametengwa kisiasa zaidi," alisema.

Lakini, Stoltenberg alionya dhidi ya kutarajia mwisho wa haraka wa vita, akisema kwamba hakuwa na dalili kwamba Putin atabadilisha njia, hata baada ya kuchaguliwa kwake tena mnamo Machi 17.

Ukraine wakati huo huo "imeonyesha kuwa wanaweza kujilinda, wanaweza kupigana kwa muda mrefu, hasa wanapopata silaha kutoka Ujerumani na washirika wengine wengi wa NATO."

Stoltenberg alikataa kuhusishwa na matarajio ya utawala wa pili wa Marekani chini ya Donald Trump, huku rais huyo wa zamani kwa sasa akiwa mbele ya wawakilishi wengine wa chama cha Republican katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura, lakini uchaguzi wa urais ukiwa umesalia karibu mwaka mmoja.

Mvutano na NATO uliongezeka wakati wa muhula uliopita wa Trump, hasa juu ya matumizi ya ulinzi. "Nina imani kwamba yeyote atakayechaguliwa kuwa rais, Marekani itaendeleza wajibu wake kwa ushirikiano wa kanda ya Atlantiki," Stoltenberg alisema.