1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya Flick, ni Nagelsmann ama Klopp?

Lilian Mtono
11 Septemba 2023

Shirikisho la soka la Ujerumani, DFB limemtimua kocha wa timu ya taifa Hansi Flick baada ya Japan kuicharaza kipigo cha fedheha cha mabao 4-1.

https://p.dw.com/p/4WBjS
Kocha wa Liverpool ya England Jürgen Klopp kama anavyoonekana kwenye picha aliyopigwa katika michuano ya Ligi ya Ulaya, 2015/2016
Kocha wa Liverpool Jürgen Klopp ni miongoni mwa makocha wenye rekodi bora na ya muda mrefu ambaye huenda akakabidhiwa kikosi cha taifa cha Ujerumani.Picha: Christopher Neundorf/firo Sportphoto/picture alliance

Shirikisho hilo limeona haliwezi kuendelea na Hansi Flick wakati taifa hilo likijiandaa kuwa mwenyeji wa michuano ya Euro mwezi Juni mwakani.

Kipigo hicho cha tatu mfululizo kimeonyesha dhahiri uwezo wa Flick, lakini aliendelea kusalia na kikosi hicho kutokana na mechi kati yao na Ufaransa inayochezwa Jumanne hii. Licha ya hayo, DFB haikuwa tayari kubeba aibu nyingine na kuamua kuachana naye.

Rais wa DFB Bernd Neuendorf amesema "Tumekubaliana kwamba timu ya taifa ya soka ya wakubwa inahitaji mwamko mpya baada ya matokeo mabovu yaliyopita. Tunahitaji ujasiri na hasa kwa kuangazia michuano ijayo ya Ulaya inayofanyika hapa. Kwangu mimi ni uamuzi mgumu sana kuwahi kuufanya nikiwa na wadhifa huu, na hasa kwa kuzingatia ninamthamini sana Hansi Flick na wasaidizi wake. "  

Flick aliisaidia Ujerumani kushinda Kombe la Dunia mwaka 2014 akiwa kocha msaidizi na aliyeshinda michezo minane ya awali baada ya tu ya kupewa kikosi cha Ujerumani mwaka 2021.

Kwa sasa shirikisho hilo la DFB linasaka kwa udi na uvumba kocha mpya, taarifa yake ilisema na kocha wa zamani wa Bayern Munich Julian Nagelsmann ndiye anayepigiwa upatu zaidi pamoja na kocha wa Liverpool, Jürgen Klopp.