1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uganda yathibitisha kupoteza wanajeshi shambulio Somalia

28 Mei 2023

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuna wanajeshi waliopoteza maisha katika shambulio lililofanywa na kundi la Al Shabaab, dhidi ya kambi ya jeshi la walinda amani wa Umoja wa Afrika kutoka Uganda nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/4Ruic
Rais Yoweri Museveni wa Uganda
Rais Yoweri Museveni wa Uganda Picha: Hannah McKay/Getty Images

Kwenye taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters, Museveni hakutaja idadi ya wanajeshi waliojeruhiwa au kuuwawa.

Akizungumzia tukio hilo, kiongozi huyo ametuma salamu za rambirambi kwa taifa na familia za waliopoteza wapendwa wao na kuongeza kwamba, jeshi tayari limeunda kamati ya kuchunguza kilichotokea.

Matamshi yake ni kauli rasmi ya kwanza kutolewa inayothibitisha kutokea kwa hasara kwa upande wa wanajeshi wa kulinda amani wa Uganda wanaowakilisha ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (ATMIS) nchini Somalia.