1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneta wa Uasin Gishu kizimbani sakata la wanafunzi Finland

Wakio Mbogho17 Agosti 2023

Seneta wa kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago pamoja na watu wengine wawili wamefikishwa mahakamani mjini Nakuru kujibu mashtaka juu ya sakata la mpango wa masomo nchini Finland unaotajwa kuwapotezea wazazi fedha.

https://p.dw.com/p/4VHdi
Symbolbild | Justiz
Picha: fikmik/YAY Images/IMAGO

Seneta wa kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago pamoja na watuhumiwa wengine wawili wamefikishwa mbele ya mahakama mjini Nakuru kujibu mashtaka kuhusu sakata la mpango wa masomo nchini Finland uliowapotezea wazazi fedha katika kaunti ya Uasin Gishu.

Washukiwa hawa wamekamatwa baada ya Rais William Ruto kuingilia kati kufuatia kilio cha muda mrefu cha wanafunzi hao.

Soma pia : Hazina: Deni la Kenya lapanda hadi kiwango cha kihistoria 

Mahakama ya Nakuru imekataa kuanza kesi hiyo ikisema kuwa mshukiwa mmoja hayuko mahakamani na ni lazima washukiwa wote wanne wafike mbele ya mahakama kabla ya mashtaka kusomwa na kesi kuanza.

Hakimu Paul Ndege ameamuru Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago na wenzake wawili waliofikishwa mahakamani waachiliwe kwa dhamana ya shilingi laki tano pesa taslimu za Kenya.

"Uamuzi huu unatolewa ukisubiri ombi la rufaa au kukamatwa kwa mshukiwa wa kwanza ambaye hayuko mahakamani. Wakati huo huo notisi ya kukamatwa kwa mshukiwa wa kwanza bado inatekelezwa."

Madai yasiyo na kikomo

Seneta Mandago ambaye ni mfuasi na rafiki wa karibu wa Rais Ruto amekuwa akiandamwa na madai hayo kuanzia mwaka uliopita.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Seneta kwenye uchaguzi mkuu uliopita alihudumu kama Gavana wa kaunti ya Uasin Gishu kwa awamu mbili, wakati huo ambapo sakata hilo la masomo nchini Finland linalogharimu shilingi bilioni 1.1 za kenya inaaminika kutekelezwa.

Hapo jana Seneta huyo aliyekuwa anasakwa na polisi alikamatwa mjini Eldoret na kusafirishwa hadi Nakuru na kukaa kizuizini, na mapema leo alifikishwa mahakamani.

Rais wa Kenya William Ruto
Rais wa Kenya William RutoPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Awali wazazi na wanafunzi waliwalalamikia na kuwakosoa viongozi hao mjini Eldoret na hata kutishia kusambaratisha kongamano la ugatuzi linalofanyika mjini humo wiki hii.

Wazazi hao wanasema baadhi ambao ni wagonjwa waliuza mali zao na sasa hawana fedha za chakula au hata dawa na wamesalia kuhangaishwa na magonjwa kama vile kisukari, kiwewe na shinikizo la damu.

Soma zaidi : Kenya: Waathirika wa mashambulizi ya ubalozi wa Marekani bado kufidiwa

Seneta Mandago na wenzake wawili wamekamatwa saa chache baada ya Rais William Ruto kuingilia kati na kutangaza hapo jana kwamba haki inapaswa kutolewa kwa wanafunzi hao.

"Sasa mambo ya uchunguzi yanaendelea, wale wote kama kuna mtu alikula hiyo pesa ajipange kulipa mapema ama ataingia taabani.  Wakati uchunguzi utamalizika mimi nitaona vile tunaweza kuwasaidia wale watoto, tutawapanga vile tunaweza kuwapatia ufadhili wa masomo hapa nyumbani, waende wasome," ameeleza rais Ruto.

Mshukiwa wa nne hajulikani aliko. Kaunti ya Elgeyo Marakwet pia imewapeleka zaidi ya wanafunzi 200 nchini Finland kwa masomo ya utabibu.