1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia azindua mkakati wa nishati safi Tanzania

George Njogopa8 Mei 2024

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amezindua mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2033.

https://p.dw.com/p/4fdEl
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais Samia anataka kuwepo nguvu ya pamoja kuanzia wahisani wa kimaendeleo, taasisi za umma na sekta binafsiPicha: Presidential Press Service Tanzania

Hatua hiyo inakuja miezi michache baada ya kiongozi huyo kuongoza mkakati kwa nchi za Afrika kuwawezesha wanawake barani humu kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, wakati aliposhiriki Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) huko Dubai.

Ndani ya mkakati huo ambao ni wa miaka 10, Rais Samia anataka kuwepo nguvu ya pamoja kuanzia wahisani wa kimaendeleo, taasisi za umma na sekta binafsi ili kuongeza chachu kufikia malengo yake:

Ikiwa sehemu ya kushajiisha uzinduzi wa mkakati  wenyewe, makundi mbali mbali ya watu wamehudhuria wakiwamo viongozi wa kisiasa, kidini, wanadiplomasia pamoja na makundi mengine kama vile madereva wa malori, mamalishe na vikundi  vingine vya wanawake ambao wanatajwa kuwa sehemu kubwa ya matumizi ya nishati isiyo rafiki.

Mkaa
Zaidi ya asilimia 90 ya kaya Tanzania hutegemea nishati chafu itokanayo na kuni, mkaa pamoja na mabaki ya kinyesi kwa kupikiaPicha: AP Photo/picture alliance

Zaidi ya asilimia 90 ya kaya nchini Tanzania hutegemea nishati chafu itokanayo na kuni, mkaa pamoja na mabaki ya kinyesi cha wanyama kwa ajili ya kupikia na shughuli nyingine za majumbani, hali ambayo wataalamu wanaonya kwamba imekuwa sehemu ya ongezeko la matatizo ya kiafya kwa wengi huku pia uharibifu wa mazingira ukivunja rekodi.

Ili kutoa mkazo kuhusu mkakati huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeanisha vipaumbele vitakavyozingatiwa kuanzia ngazi ya kaya mpaka taifa.

Ripoti zinaonyesha kwamba kila mwaka nchini Tanzania watu 33,000 hupoteza maisha kutokana na mikasa inayosababishwa na matumizi ya nishati isiyo salama, na kiwango hicho kinadhihiri zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwepo wa nishati safi na salama ya kupikia bado ni ndogo.

Serikali imepanga bajeti ya shilingi trilioni 4.6 kwa ajili ya kufanikisha mkakati huo ikiwamo usambazaji wa nishati safi katika maeneo mbalimbali ya nchi hasa huko vijijini. 

Rais Samia anataka ifikapo baadaye mwaka huu mamlaka za kiutendaji kuanza kutoa ripoti juu ya utekelezaji wa mkakati huo ambao unakuja huku tayari baadhi ya taasisi zinazokusanya watu wengi  kama vile majeshi na shule zikiwa zimeanza kutumia nishati safi na salama ya kupikia.