1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchini China, Baerbock asema maoni ya Macron ni ya Ulaya

Daniel Gakuba
13 Aprili 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Ulaya inao mtazamo sawa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, juu ya uhusiano baina ya Ulaya na China. Vile vile ameonya dhidi ya kupanuka kwa mzozo wa Taiwan.

https://p.dw.com/p/4Q1G4
China Aussenministerin Annalena Baerbock in Tianjin
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akizungumza nchini ChinaPicha: Kira Hofmann/photothek/IMAGO

Annalena Baerbock ni mwanasiasa mwingine wa ngazi za juu wa Ulaya kuitembelea China katika muda wa siku chache zilizopita. Baada ya kuwasili katika mji wa Tianjin Alhamisi, waziri huyo ameunga mkono kauli iliyosababisha utata ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Soma zaidi: Macron: Ulaya haipaswi kujitenga na China

Katika kauli hiyo, Rais Macron alisema Ulaya inapaswa kuwa na sera yake juu ya China na Taiwan badala ya kufuata tu Marekani. Baada ya matamshi hayo rais huyo wa Ufaransa alikabiliwa na mashambulizi makali kutoka Marekani na washirika ndani ya Ulaya.

Akijibu ukosoaji huo dhidi ya Rais Macron, Baerbock amesema anataka kusisitiza kuwa sera ya Ufaransa kuhusu China ni taswira sahihi ya sera ya Ulaya.

Waziri huyo wa Ujerumani ameongeza kuwa ''nguvu ya Umoja wa Ulaya haitokani tu na kuwa nchi wanachama ziko karibu, lakini pia zinatokana na ukweli kuwa zinafuata mkakati mmoja kuhusu masuala ya msingi kwa maslahi na maadili yao.''

Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, matamshi yake kuwa Ulaya iache kuifuata tu Marekani yamemtia matataniPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Taiwan, mwiba katika uhusiano baina ya Ulaya na China

Hali kadhalika Bi Annalena Baerbock ameonya juu ya mzozo wa Taiwan, na madhara unaoweza kusababisha katika uhusiano kati ya China na Ulaya.

Soma zaidi: Ujerumani yatoa wito wa kupunguzwa kwa mivutano ya China na Taiwan

Amesema, ''kuongezeka kwa uhasama wa kijeshi katika ujia wa bahari wa Taiwan kutakuwa na athari mbaya kabisa kwa dunia, na kutaiathiri kwa njia ya kipekee Ujerumani ambayo ni nchi ya viwanda.''

Mwanasiasa huyo amesema asilimia 50 ya biashara ya dunia inapita katika ujia huo wa bahari, na asilimia 70 ya bidhaa za kitaalamu zijulikanazo kama ''semiconductor'' zinapita katika ujia huo huo.

''Uhuru katika njia hiyo ni wa maslahi makubwa kwa uchumi wetu, ameongeza.

USS Milius-Schiff
Mvutano baina ya China na Taiwan unatishia usalama wa biashara ya duniaPicha: Omar-Kareem Powell/AFP

China kuzuia shughuli katika bahari karibu na Taiwan

Huku hayo yakiarifiwa, China imesema itapiga marufuku vyombo vya usafiri wa majini katika eneo la bahari karibu na kisiwa cha Taiwan siku ya Jumapili, kuepusha madhara yatokanayo na vipande vya mitambo ya kurushia satelaiti.

Soma zaidi: China yahitimisha luteka za kijeshi kuizunguka Taiwan

Marufuku hiyo imewekwa kukiwa na hali tete kati ya China na Taiwan, baada ya China kufanya luteka kubwa za kijeshi kama jibu kwa hatua ya rais wa Taiwan Tsai Ing-wen kufanya mazungumzo wa spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Kevin McCarthy jimboni California.

China inaichukulia Taiwan kama eneo lake na inapiga vikali maingiliano kati ya uongozi wa kisiwa hicho na viongozi wa nchi nyingine. Kwa upande wake Taiwan inayapinga madai hayo ya China, ikidai uhuru wake.

 

Chanzo: zc, ab/msh (dpa, Reuters)