1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Umoja wa Ulaya kuweka sheria kali za uhamiaji.

Zainab Aziz
9 Juni 2023

Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya wamekubaliana juu ya mapendekezo ya mageuzi yatakayoleta sheria kali katika taratibu za uhamiaji baada ya mkutano wao uliofanyika Luxembourg.

https://p.dw.com/p/4SO8l
Luxembourg EU-Minister Migrationsabkommen
Picha: RTRTV

Mawaziri hao wameafikiana juu ya mpango ambapo nchi wanachama, ama zikubali kuwapokea wahamiaji wanaoomba hifadhi au zikubali kulipia katika mfuko wa wakimbizi unaosimamiwa na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya. Nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekubalina juu ya mpango wa kuweka sheria kali kwa wanaoomba kuhamia katika nchi hizo. Mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi hizo walikutana ili kuyapitisha mageuzi ya kina kirefu juu ya taratibu za uhamiaji.

Kulingana na makubaliano waliyofikia, kwa mara ya kwanza taratibu za kuomba uhamiaji zitakamilishwa nje ya mipaka ya nchi za Ulaya hivyo basi watu wanaotoka kwenye nchi zinazozingatiwa kuwa salama na ambao hawana matumaini ya kupata hifadhi hawataruhusiwa kuingia barani Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy FaeserPicha: Nadja Wohlleben/REUTERS

Kwa mujibu wa makubaliano hayo vitawekwa vituo karibu na mipaka ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya watu wanaoomba kuhamia barani Ulaya. Ikiwa mwombaji hana matumaini kabisa ya kukubaliwa kuingia Ulaya baada ya uchunguzi wa muda wa wiki mbili atarudishwa kwao.

Kulingana na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya muda wa kusubiri kwa watu wanaoomba kuhamia Ulaya ni miezi sita tu. Juu ya mpango huo wa mageuzi uliopitishwa na mawaziri wa mambo ya ndani waliokutana Luxembourg, Sweden imesema  maamuzi yaliyopitishwa ni ya kihistoria. Sweden kwa sasa ndiyo rais wa zamu wa Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki.
Waziri Mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki.Picha: Piotr Nowak/PAP/picture alliance

Hata hivyo Poland haikubaliani na kipengele kinachohusu kuchangia katika mfuko wa kugharimia wahamiaji na wala  haikubaliani na wazo la kuwapokea wahamiaji. Waziri mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki ameeleza kuwa nchi yake haitakubali kulipa kwa lazima kwa sababu ya kukataa kuwapokea wahamiaji. Amesema msimamo wao hautabailika. Morawiecki ameeleza kuwa Poland imewapokea mamilioni ya wakimbizi kutoka Ukraine na kwamba imeonesha msimamo thabiti katika hilo na pia itaonyesha msimamo thabiti dhidi ya uhamiaji bandia. Waziri mkuu wa Poland amesema serikali yake haitawaruhusu wahalifu wanaosafirisha watu kuiambia Poland nini cha  kufanya.

Bunge la Ulaya .
Bunge la Ulaya.Picha: Johanna Geron/REUTERS

Mageuzi hayo pia yamekosolewa na Austria, Uholanzi na Italia. Nchi hizo tatu zimesema mageuzi hayo yaliyopendekezwa hayatoshi. Lakini Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Faeser amesema makubaliano yaliyofikiwa ni mafanikio ya kihistoria kwa Umoja wa Ulaya. Baada ya mawaziri wa Ulaya kufikia hatua hiyo, mazungumzo na bunge la Ulaya yataanza hatahivyo hakuna uhakika wa  kuukamilisha mchakato wote kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge hilo mwaka ujao.

Chanzo:DPA