1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu waanza Algeria

1 Novemba 2022

Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wanakutana mjini Algiers nchini Algeria kwa mkutano wa kilele utakaogubikwa na misuguano miongoni mwa nchi wanachama pamoja na masuala chungunzima yanayougawa ulimwengu wa kiarabu.

https://p.dw.com/p/4IuqA
Saudi-Arabien Riyadh | Palast | Gulf Cooperation Council
Picha: Bandar Aljaloud/Saudi Royal Palace/AP/picture alliance

Mkutano huo wa kilele unaoanza leo Novemba 1 na kuendelea hadi Novemba 2 unawakutanisha kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019 viongozi wa Jumuiya ya nchi za kiarabu yenye wanachama 22.

Mkutano wa mwisho  ulifanyika kabla ya kuzuka janga la virusi vya corona na hata kabla ya mabadiliko makubwa ya kisera kwa baadhi ya nchi wanachama kuelekea Israel.

Tangu wakati huo mambo mengi yamechukua mkondo tofauti, janga la virusi vya corona ni kama limedhibitiwa lakini kuna changamoto mpya ya vita nchini Ukraine na kuendelea kutanuka kwa orodha ya nchi wanachama zilizoamua kurekebisha au kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Israel, taifa ambalo limekuwa sababu ya mshikamano wa mataifa ya kiarabu kwa miongo mingi.

Palestinian factions sign reconciliation agreement in Algeria
Picha: Fazil Abd Erahim /AA/picture alliance

Ama kuhusu mikataba ya kurekebisha mahusiano na Israel iliyotiwa saini na mataifa ya UAE, Bahrain, Sudan na Morocco hilo limesababisha mgawanyiko wa pande mbili ndani ya ulimwengu wa kiarabu. 

Algeria, iliyo mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu ni miongoni mwa mataifa yanayopinga vikali mikataba hiyo, ikiamini kuwa italemaza kabisa juhudi za kuisaidia Palestina kwenye mzozo wa Mashariki ya Kati.

Serikali mjini Algiers inatarajiwa kulitumia jukwaa hilo la siku mbili kusisitiza uungaji wake mkono kwa Wapalestina na kuendeleza ukosoaji wake kwa mataifa yaliyoinyooshea Israel mkono wa urafiki.

Mivutano ya ndani na mzozo wa Ukraine kugubika majadiliano

Kadhalika kuna mivutano mikubwa miongoni mwa nchi wanachama. Na ulio wazi kabisa ni ule kati ya Algeria na jirani yake Morocco, msuguano uliofikia hatua ya mataifa hayo mawili kusitisha mahusiano yao ya kidiplomasia.

Flash-Galerie Bildergalerie Das bewegte die Welt im Jahr 2011 Jahresrückblick international 2011
Picha: AP

Liko pia suala la Syria na iwapo nchi hiyo inafaa kukaribishwa tena ndani ya Jumuiya ya nchi za kiarabu baada ya muongo mmoja wa kutengwa kutokana na lawama kwamba ilitumia nguvu kuwakabili waandamanaji wakati wa vuguvugu la kudai mageuzi lililoanza mwaka 2011.

Mizozo nchini Yemen, Sudan na Libya yumkini hiyo nayo itajadiliwa katika mkutano huo wa mjini Algiers.

Inatazamiwa suala la mzozo wa upatikanaji chakula duniani na kupanda kwa gharama za nishati tangu kuzuka kwa vita nchini Ukraine nalo vilevile litawekwa mezani.

Mizozo hiyo imeziathiri pakubwa nchi nyingi za Jumuiya hiyo ikiwemo Misri, Lebanon na Tunisia zinazotaabika kupata chakula cha kutosheleza mahitaji ya ndani.

Je, viongozi watamudu kuzika tofauti zao?

Changamoto kubwa kwenye mkutano huo wa Algiers itakuwa ni kuandaliwa kwa tamko la pamoja la viongozi wanaohudhuria.

Wachambuzi wengi wa masuala ya siasa wanaamini itakuwa vigumu kupatikana mwafaka ya kipi kiandikwe ndani ya tamko hilo au lugha gani itumike kueleza kilichoafikiwa.

Viongozi kadhaa vigogo wa ulimwengu wa kiarabu tayari wamethibitisha hawatohudhuria mkutano huo.

Miongoni mwao ni mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia na Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco. Viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain nao pia wamechagua hawatokwenda mjini Algiers.