1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCyprus

Misaada ya kwanza kwa njia bahari yasubiriwa Ukanda wa Gaza

9 Machi 2024

Boti iliyobeba msaada unaosubiriwa kwa shauku kwenye Ukanda wa Gaza inapeleka shehena ya kwanza kutokea Cyprus.

https://p.dw.com/p/4dL0k
Bandari ya Larnaca | Cyprus | Msaada kwa Gaza
Tani 200 za mchele na unga wa ngano zimepakiwa kwenye meli inayokwenda Gaza.Picha: Marcos Andronicou/AP/dpa/picture alliance

Inafanya safari hiyo muhimu katika wakati Umoja wa Mataifa umetahadharisha juu ya kukaribia viwango vya baa la njaa kwenye Ukanda wa Gaza.

Tahadhari hiyo imetolewa katikati mwa mapigano yaliyochacha kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa kundi la Hamas.

Meli ya hisani ya Marekani iitwayo, World Central Kitchen, imeshusha shehena ya misaada na kuipakia kwenye boti nyingine huko Cyprus tayari kwa safari ya kuelekea Gaza.

Shughuli hizo zinatumia bandari ya Larnaca na kisha shehena za misaada zitafikishwa kaskazini mwa Gaza.

"Chombo chetu kipo tayari kuanza safari tutakapopewa ruhusa," imesema taarifa ya asasi ya Open Arms, mojawapo kati ya taasisi nyingi za hisani zinazoshiriki juhudi za kufikisha misaada ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza.

Njia ya bahari inalenga kukwepa vizuizi vya njia ya ardhini 

Mpango wa kutumiwa njia ya bahari kufikisha misaada Gaza unaratibiwa kwa pamoja na Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa wengine washirika.

Ulitangazwa kwa mara ya kwanza na rais Joe Biden alipotoa hotuba yake ya kila mwaka ya hali ya taifa usiku wa kuamkia Ijumaa.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen aliyekuwa ziarani nchini Cyprus alifuatia kutoa tamko kwamba msaada wa kwanza ungepelekwa Gaza mwishoni mwa juma hili.

Ukanda wa Gaza | Misaada ya kiutu iliyorushwa kutoka kwenye ndege
Njia ya kupeleka misaada kwa kutumia ndege na maparashuti haikusaidia sana kufikisha msaada wa kutosha huko GazaPicha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Njia ya kutumia bahari kupitia Cyprus -- taifa la Umoja wa Ulaya lililo karibu zaidi na Ukanda wa Gaza -- inalenga kuepuka vikwazo vya kutumia njia ya ardhini, ambayo maafisa wa misaada ya kiutu na serikali za mataifa ya magharibi wameilaumu Israel kwamba inaiwekea vizingiti.

Kwa zaidi ya miezi mitano tangu kuzuka kwa vita wakaazi milioni 2.4 wa Ukanda wa Gaza wanataabika kwa kukosa huduma muhimu hususani wale wanaoishi upande wa kaskazini, eneo ambalo operesheni ya ardhini ya jeshi la Israel ilianzia.

Jitihada za hapo kabla za kutuma misaada ya ziada kwa njia ya anga hazijafua dafu na mashirika ya kimataifa yameendelea kutoa tahadhari kwamba umma wa Gaza unakabiliwa na hali mbaya.

Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza inayoongozwa na kundi la Hamas, imesema watoto watatu zaidi wamepoteza maisha kutokana na utapiamlo na ukosefu wa maji mwilini. Idadi hiyo inafanya jumla ya watoto waliokufa hadi sasa kwa sababu hizo kufikia 23.

Mapigano bado ni makali huku idadi ya vifo huko Gaza yafikia 30,960

Mapigano pia bado yanaendelea kwenye eneo hilo na hapo jana watu 82 waliuwawa kutokana na mashambulizi ya anga na ya ardhini ya majeshi ya Israel.

Kwa jumla wizara ya afya inasema hadi sasa watu 30,960 wengi wakiwa watoto na wanawake wameuawa tangu kuzuka kwa vita.

Hali ya Ukanda wa Gaza
Hali ya Ukanda wa Gaza Picha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Vita hivyo vilizuka mwisho mwa mwaka jana baada ya kundi la Hamas kufanya shambulizi kubwa ndani ya Israel mnamo Oktoba 7 na kusababisha vifo vya watu 1,200.

Licha ya jitihada za kutafuta makubaliano mapya ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili, hadi siku ya Jumamosi jioni dalili hazikuwa zimeonekana.

Rais Joe Biden ambaye aliahidi kwamba mkataba wa kusitishwa vita utakapitikana siku za karibuni, alisema hadi sasa uwezekano wa hilo kutokea "bado ni mgumu".

Kulikuwa na malengo ya kufanikisha usitishaji wa muda wa mapigano kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhan unatarajiwa kuanza siku ya Jumapili au Jumatatu