1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka ICJ kutoiamuru Israel kukomesha ukaliaji

Iddi Ssessanga
21 Februari 2024

Marekani imeiambia Mahakama ya Umoja wa Mataifa Jumatano, kwamba Israel haipaswi kulazimishwa kisheria kuondoka katika ardhi ya Wapalestina inayoikalia kwa mabavu bila hakikisho la usalama.

https://p.dw.com/p/4chrl
Uholanzi The Hague | Mahakama ya Kimataifa ya Haki | Kesi ya mauaji ya kimbari ya Israel | Waandamanaji
Mahakama ya ICJ inasikiliza maoni y amataifa kuhusu ukaliaji wa Israel wa ardhi za Wapalestina.Picha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

Mahakama hiyo ya kimataifa ya haki, ICJ, inaendesha vikao kwa muda wa wiki moja, kufuatia ombi la Umoja wa Mataifa kuitaka itoe maoni ya ushauri, ambapo mataifa 52  yanatoa mitazamo yake kuhusu ukaliaji wa kimabavu wa Israel wa ardhi za Wapalestina.

Wazungumzaji wengi waliokwisha toa maoni yao mbele ya mahakama hiyo ya juu ya Umoja wa Mataifa wametaka Israel ikomeshe ukaliaji wake, uliyofuatia vita vya siku sita kati yake na mataifa ya Kiarabu mwaka 1967, lakini Marekani imekuja kumtetea mshirika wake katika mahakama hiyo.

Kaimu mshauri wa masuala ya kisheria katika Wizara ya Mambo ya Nje Richard Visek amesema jopo la majaji 15 wa ICJ halipaswi kutafuta kusuluhisha mzozo wa miongo kadhaa kati ya Israel na Palestina "kupitia maoni ya ushauri yaliyoshughulikiwa kwa maswali yanayoangazia vitendo vya upande mmoja pekee."

Soma pia: Vita vya Israel-Hamas vyazua mvutano tamasha la Berlinale

"Mahakama haipaswi kugundua kuwa Israel inawajibu wa kisheria kujiondoa mara moja na bila masharti kutoka eneo linalokaliwa," alisema Richard Visek, mshauri wa sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

"Sote tulikumbushwa kuhusu mahitaji hayo ya usalama mnamo Oktoba 7," alisema, akimaanisha mashambulizi ya Hamas ambayo yalizua mzozo wa sasa.

Umoja wa Mataifa umeitaka ICJ kutoa "maoni ya ushauri" kuhusu "matokeo ya kisheria yanayotokana na sera na matendo ya Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Jerusalem Mashariki".

Uholanzi The Hague| Mahakama ya Umoja wa Mataifa| Kesi dhidi ya Israel
ICJ inatazamiwa kutoa hukumu yake isiyofungamanisha kisheria baadae mwaka huu.Picha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Pengine mahakama hiyo itatoa maoni yake kabla ya mwisho wa mwaka, lakini hayafungamanishi kisheria.

Palestina: Tulitaraji zaidi ya hilo kutoka kwa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyad al-Maliki aliwaambia waandishi wa habari baada ya taarifa ya Marekani: "Nilitarajia mengi zaidi. Sikusikia lolote jipya."

Washington imekuwa ikisisitiza kwamba mzozo wa Israel na Palestina ushughulikiwe katika "majukwaa mengine na sio hapa", Al-Maliki alisema.

"Ndiyo, tulijaribu vikao vingine kwa miaka 75 iliyopita na tulikabiliana na kura ya turufu ya Marekani na ubabe wa Marekani juu ya michakato ya kufanya maamuzi ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa," alisema.

"Na ndio maana tulikuja ICJ."

Israel haishiriki katika vikao vya usikilizaji wa shauri hilo, lakini iliwasilisha mchango wake wa maandishi ambamo iliyaelezea maswali iliyoulizwa mahakama hiyo kuwa ya chuki na upendeleo.

Visek, ambaye amezungumza katika siku ya tatu ya vikao vya ICJ, amesema mahakama hiyo inaweza kushughulikia maswali yaliyo mbele yake ndani ya mfumo uliowekwa kwa kuzingatia kanuni ya ardhi ya amani na ndani ya vigezo vya kanuni zilizowekwa za sheria ya ukaliaji.

"Hatua zozote kuelekea Israel kujiondoa kutoka Ukingo wa Magharibi na Gaza zinahitaji kuzingatia mahitaji halisi ya usalama ya Israeli," alisema.

Marekani New York | Baraza la Usalama la UN | Mjadala kuhusu Mashariki ya Kati | Riyad al-Maliki, Mamlaka ya ndani ya Wapalestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Wapalestina Riyad al-Maliki amesema hajashangazwa na kauli za Marekani ICJ.Picha: Shannon Stapleton/REUTERS

Mashambulizi ya Oktoba 7 na ghasia zinazoendelea katika Ukanda wa Gaza "zinaimarisha azimio la Marekani la kufikia haraka amani ya mwisho," Visek alisema.

Misri yataka haki ya Wapalestina kujiamulia mambo yao

Akizungumza leo pia, mwakilishi kutoka Misri, ambayo imekuwa na jukumu muhimu katika mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina, amesema ukaliaji huo ni muendelezo wa ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Soma pia: Je, Palestina inayotambulika itasaidia kumaliza mzozo wa Gaza?

"Matokeo ya ukaliaji wa muda mrefu wa Israeli yako wazi na hakuwezi kuwa na amani, hakuwezi kuwa na utulivu, hakuwezi kuwa na ustawi bila kuzingatia utawala wa sheria," mshauri wa sheria wa wizara ya mambo ya nje Jasmine Moussa alisema.

Vikao hivyo vilianza Jumatatu kwa saa tatu za ushahidi kutoka kwa maafisa wa Palestina, ambao waliishtumu Israel kwa kuendesha mfumo wa ukoloni na ubaguzi wa rangi na utengano - Apartheid.

Al-Maliki alikuwa amewataka majaji kutoa wito wa kukomesha ukaliaji huo "mara moja, kabisa na bila masharti".

Balozi wa Afrika Kusini nchini Uholanzi aliiambia mahakama kwamba sera za Israel "zimekuwa mbaya zaidi" kuliko ubaguzi na utengano waliopitia Waafrika Kusini weusi kabla ya 1994.

Kesi hiyo ni tofauti na kesi kubwa iliyoletwa na Pretoria dhidi ya Israel kwa madai ya mauaji ya halaiki wakati wa mashambulizi yake ya sasa huko Gaza.

Katika kesi hiyo, ICJ iliamua kwamba Israel inapaswa kufanya kila iwezalo kuzuia vitendo vya mauaji ya halaiki huko Gaza na kuruhusu misaada ya kibinadamu.

Israel | Knesset Jerusalem Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa israel Benjamin Netanyahu ameapa kutorusu kuundwa kwa upande mmoja kwa taifa la Palestina.Picha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Tamko la Israel kupingwa taifa la Palestina

Msimamo wa Israel unasema makubaliano yoyote a kudumu na Wapalestina yanapaswa kufikiwa kwa njia ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande mbili na siyo kupitia shinikizo la kimataifa.

Bunge la nchi hiyo la Knesset, limepiga kura kwa wingi siku ya Jumatano kuidhinisha tamko la serikali ya waziri mkuu Netanyahu Benjamin Netanyahu, la wiki iliyopita, kupinga jaribio lolote la upande mmoja la kuundwa kwa taifa la Palestina.

"Knesset ilikuja pamoja kwa wingi mkubwa dhidi ya jaribio la kutulazimisha kuanzishwa taifa la Palestina, ambalo sio tu kwamba lingeshindwa kuleta amani bali litahatarisha taifa la Israel," alisema Netanyahu.

Suluhu la mataifa mawili kwa muda mrefu limekuwa sera ya msingi ya mataifa ya magharibi katika kanda ya Mashariki ya Kati. Tangu kuzuka kwa vita vya Gaza mwezi Oktoba, Marekani imekuwa ikijaribu kuibua hoja ya hatua kuelekea kuundwa kwa taifa la Palestina kama sehemu ya mapatano mapana ya Mashariki ya Kati ambayo yatajumuisha Saudi Arabia na mataifa mengine ya Kiarabu kurekebisha rasmi uhusiano na Israel.