1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, NATO watoa jibu la maandishi kwa masharti ya Urusi

Daniel Gakuba
27 Januari 2022

Marekani najumuiya ya kujihami ya NATO wamewasilisha jibu la maandishi kwa masharti ya Urusi kuhusu usalama wake, huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akisema hawakuridhia chochote.

https://p.dw.com/p/469YF
USA Außenminister Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony BlinkenPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Masharti makubwa ya Urusi yaliyohitaji majibu ya maandishi, ni kutaka kuhakikishiwa kuwa Ukraine kamwe haitapewa uanachama wa NATO, na kwamba jumuiya hiyo ya kiulinzi haitaendelea kujitanua upande wa mashariki.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema majibu waliyoyapeleka yanazingatia wasiwasi wa Urusi na kujumuisha kero za Marekani na washirika wake, lakini hayakuridhia chochote.

Tayari kwa heri au shari

Mwanadiplomasia huyo amesisitiza kuwa yaliyomo katika ujumbe huo wa maandishi kwa Urusi yatabakia kuwa siri, kwa sababu ni kwa njia hiyo diplomasia inaweza kupata ufanisi, na kuongeza kuwa sasa kazi imebaki upande wa Urusi.

Militärübung in Russland
Urusi imerundika wanajeshi na zana nzito za kivita karibu na mpaka wa UkrainePicha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/dpa/picture alliance

Amesema, ''Kwa sasa waraka tumewafikishia na mpira uko katika uwanja wao,'' na kuongeza kuwa ikiwa Urusi itachagua diplomasia na mjadala, au wataamua kuendeleza ubabe dhidi ya Ukraine, ''sisi tuko tayari kwa yote.''

Juu ya ujumbe huo wa maandishi kwa Urusi, waziri Blinken amesema anatarajia kukutana tena na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov mnamo siku za hivi karibuni.

NATO pia yataka suluhu ya amani

Wakati huo huo, katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ameunga mkono pia mazungumzo na diplomasia kama njia ya kuutanzua mzozo wa Ukraine, yeye pia akionya kuwa ikiwa heri itashindikana wako tayari kwa shari.

Urusi haijajibu chochote kuhusu majibu hayo ya maandishi ya Marekani na NATO, lakini awali waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov aliwaambia wabunge mjini Moscow, kuwa ikiwa matakwa yao hayatopata jibu muafaka, Urusi itachukua hatua zinazohitajika za ulipizaji kisasi.

Blinken und Lawrow, Ukraine Gespräche in Genf
Antony Blinken (kushoto) na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov walipokutana mjini Geneva tarehe 21.01.2022Picha: Pavel Bednyakov/Sputnik/picture alliance/dpa

Mataifa makubwa ya Ulaya yapigia debe mazungumzo

Huku haya yakijiri, Ufaransa na Ujerumani zinaendesha juhudi za kidiplomasia kutafuta suluhu ya mzozo huu baina ya Urusi na Ukraine. Hapo jana, wajumbe wa nchi hizo walishiriki katika mazungumzo yaliyowahusisha wawakilishi wa Urusi na Ukraine mjini Paris, chini ya mpango ujulikanao kama Normandy.

Baada ya mazungumzo hayo yaliyodumu kwa masaa manane, mkuu wa ofisi ya Rais wa Ukraine Andriy Yermak alisema kitu kizuri kilichodhihirika ni kwamba pande zote zinao utashi wa kujitolea kuumaliza mgogoro huo.

China nayo imeingilia katika katika mvutano huo, ikisema ni lazima masharti ya Urusi, ambayo china imesema yanaeleweka, yatiliwe maanani na kila upande katika mzozo huo. Wizara ya mambo ya nje ya China imesema hayo yametiliwa mkazo na waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Marekani, Antony Blinken.

afpe, dpae