1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baadhi ya makundi ya wapiganaji yajisalimisha Kongo

Bruce Amani
30 Januari 2024

Mamia ya wanachama wa kundi linalojiita la ulinzi wa jamii wamejisalimisha kwa jeshi la Kongo na kusaini kile kilichosemekana muafaka wa amani wa upande mmoja, katika eneo lenye machafuko la kaskazini mashariki mwa nchi.

https://p.dw.com/p/4bols
Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Wanachama wa makundi ya wapiganaji
Wanachama wa makundi ya wapiganaji wakiwa chini ya ulinzi wa jeshi la Kongo, katika eneo la Goma.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mwandishi habari mmoja wa AFP amesema kundi hilo lenye vijana wengi liliwasili katika mji mkuu wa mkoa huo, Bunia wakitumia magari kadhaa wakiwa wamevalia nguo za kiraia na bila ya silaha.

Msemaji wa kundi hilo linalojiita Zaire, Jean-Marie Ngadjole amesema wamedhamiria na wako tayari kujiunga na mchakato wa amani na kushiriki katika mpango wa utangamano wa jamii utakaoongozwa na mamlaka za Kongo. 

Soma pia:Takriban raia 20 wauawa kwenye shambulizi nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo

Kundi hilo lilisema ni sehemu ya kundi la ulinzi lililoundwa mwaka wa 2019 kuyalinda maslahi ya jamii tano ambazo zimekuwa waathiriwa wa ukatili unaofanywa katika mkoa wa Ituri karibu na mpaka na Uganda.

Kundi hilo linalojulikana kama "Zaire" linasema linawakilisha jamii za Hema, Mambisa, Alur, Akongo-Nyali na Ndo-Okebu na ni mpinzani wa Codeco, kundi la wapiganaji wanaosema dhamira yao ni kulinda kabila la Lendu dhidi ya Hema na washirika wao.