1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu Zainab Aziz
17 Mei 2024

Kati ya masuala ya Afrika yaliyopewa umuhimu na magazeti ya Ujerumani wiki hii ni juu ya hukumu ya miaka 20 jela kwa aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Gambia Ousman Sonko.

https://p.dw.com/p/4fzv7
Magazeti ya Ujerumani
Magazeti ya UjerumaniPicha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neuer Zürcher wiki hii liliandika kuhusu hukumu ya miaka 20 jela iliyotolewa kwa aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Gambia Ousman Sonko chini ya utawala wa Yahya Jammeh. Hukumu hiyo ilitolewa baada ya  Mahakama ya Uhalifu ya Shirikisho la Uswisi mjini Bellinzona kumkuta na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Sonko alihukumiwa Jumatano baada uchunguzi wa Mwanasheria Mkuu na kesi iliyodumu kwa miezi kadhaa. Januari 2017, Ousman Sonko alikamatwa akiwa katika makazi ya waomba hifadhi kwenye jimbo la Bern nchini Uswisi. Alikamatwa baada ya mmoja wa raia wa Gambia kumtambua. Matokeo yake, shirika moja la haki za binaadamu  lenye makao yake mjini Geneva lilimfungulia mashtaka. 

Gazeti hiyo linaongeza kuwa, kesi yake katika ofisi ya mwanasheria mkuu ilidumu kwa zaidi ya miaka sita. Katika kesi hiyo Sonko alituhumiwa kwa makosa kadhaa yakiwemo mauaji, utesaji na ubakaji na mahakama imethibitisha kuwa aliyatenda makosa hayo. Kulingana na mahakama hiyo, Ousman Sonko, alitenda mengi kati ya makosa hayo mwenyewe na mengine yalifanywa na jeshi la siri chini ya amri yake.

die tageszeitung

Mwanzoni mwa juma, die tageszeitung, liliandika kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais wa Chad ambapo tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Mahamat Déby kuwa alishinda kwa kishindo katika  kinyang'anyiro hicho kwa kupata asilimia 61.3 ya kura zote.

Mpinzani wake mkuu Waziri Mkuu Succès Masra hakubaliani na ushindi huu licha ya kuambulia asilimia 18.3 ya kura. Kimsingi, matokeo ya urais yalitazamiwa kutolewa walau baada ya wiki mbili. Badala yake, mamlaka hiyo ilihitaji siku tatu tu kutoa matokeo hayo.

die tageszeitung limefafanua kuwa, uchaguzi huo ulikuwa na dosari nyingi. Hakukuwa na waangalizi huru wa uchaguzi. Kinyume na ahadi ya awali vibali kwa waangalizi 2900 wa uchaguzi wa Chad vilikataliwa kutolewa dakika za mwisho.  Mawakala wa upinzani walikataliwa kushiriki katika kuhesabu kura.

Kwa hivyo matokeo hayakuthibitishwa na upande mmoja na ndiyo maana matokeo yalitolewa haraka ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika ambazo huhitaji wiki kadhaa kukamilisha shughuli hiyo. Licha ya hayo yote, Deby sasa ni Rais mteule, Haifahamiki hasa ni nini kitampata aliyekuwa waziri mkuu Masra, lakini anabaki kuwa mwanasiasa mwenye nguvu nchini Chad na taifa hilo nalo linasalia kuwa na mgawanyiko baada ya uchaguzi huo.

NZZ  am Sonntag

NZZ am Sonntag lilimulika kurejea ulingoni kisiasa kwa aliyewahi kuwa rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma, likimfananisha na aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump.

Gazeti hilo linabainisha kuwa, hakuna jina linalohusishwa na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka kama la Jacob  Zuma  nchini Afrika ya Kusini. Pamoja na hilo, Zuma, aliyewahi kuwa kiongozi wa chama tawala cha African National Congress (ANC) anarejea kwenye ulingo wa siasa.

Lengo la Zuma mwenye miaka 82 liko wazi: Kulipa kisasi kwa chama chake cha zamani kupitia chama chake kipya cha Umkhonto we Sizwe (MK), kilichoanzishwa miezi michache iliyopita. Analipa kisasi  kwa Rais wa sasa Cyril Ramaphosa, ambaye kwa tahadhari kubwa alijitenga naye na kufanikiwa kuivuta upande wake kambi ya Zuma ndani ya ANC.

NZZ am Sonntag liliandika, sawa na Donald Trump, Zuma mwenye kipaji cha muziki, pia ni mburudishaji anapokuwa kwenye jukwaa la kampeni. Huteka mioyo ya hadhira yake.

Hadi sasa haifahamiki ikiwa ataruhusiwa hata kuingia bungeni licha ya kuwa chaguo namba moja la chama chake cha MK. Miaka mitatu iliyopita alihukumiwa miezi 15 jela baada ya kukaidi wito wa mahakama. Zuma, alitumikia kifungo hicho kwa miezi mitatu pekee. Alisamehewa na hukumu yake ilifupishwa kutokana na kile kinachodaiwa kuwa sababu za kiafya.

Jacob Zuma
Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini Jacob Zuma akiwahutubia wafuasi wa chama chake kipya cha MKPicha: AP/picture alliance

Kwa mujibu wa sheria za Afrika ya Kusini wavunja sheria waliohukumiwa zaidi ya mwaka mmoja jela hawaruhusiwi kugombea ubunge kwa miaka mitano. Amewaahidi wafuasi wake kuwa watashinda kwa zaidi ya theluthi mbili, jambo ambalo ni gumu kutekelezeka

Lakini kwa vyovyote vile huenda Zuma akapata nafasi tena katika siasa za Afrika Kusini, ndiyo maaana wanamuita mtu mwenye roho tisa.

die tageszeitung

die tageszeitung liliangazia uwezekano wa timu ya soka ya wanawake ya Zambia kutoshiriki michezo ya Olimpiki nchini Ufaransa

Limeandika timu hiyo ina sababu ya kuwa na wasiwasi wa kushiriki katika michezo hiyo itakayofanyika mjini Paris.  Kwanza kabisa linayataja mafanikio ya timu hiyo yakiwemo kufuzu katika michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka 2021. Ilishiriki pia katika kombe la dunia la wanawake lililofanyika mwaka jana huko Australia na New Zealand.  die tageszeitung limeandika mengi, lakini linaeleza kuwa, kuna hofu huenda timu hiyo ikapokwa matunda ya kazi yake katika mashindano yajayo ya Olimpiki.

Linaeleza kuwa, maafisa wa chama cha soka cha Zambia wamekuwa sehemu kuu ya uchunguzi wa tuhuma za rushwa. Rais wa chama hicho Andrew Kamanga anatuhumiwa kutumia fedha za serikali kwa kujinufaisha na kugharamia safari za maafisa kwenda kwenye michuano ya soka la wanaume kwa mataifa ya Afrika AFCON nchini Ivory Coast.

Kwa shirikisho la soka ulimwenguni FIFA, hili linaashiria kuwa huenda kulikuwa na ushawishi wa serikali katika soka, suala linaloweza kusababisha Zambia isimamishwe uanachama wake kwenye shirikisho hilo. Matokeo yake, timu hiyo ya wanawake ya Zambia inaweza isishiriki Olimpiki na tayari chama cha soka cha Zambia kimeandikiwa barua na FIFA kuhusu uwezekano wa kuadhibiwa.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen