1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko, maporomoko yasomba nyumba kadhaa Kenya

Tatu Karema
30 Aprili 2024

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya inasema mafuriko na maporomoko ya ardhi yamesomba nyumba na kukatiza shughuli katika eneo la Mahi-Mahiu, huku watu 45 wakifariki dunia na wengine wakiwa hawajulikani walipo.

https://p.dw.com/p/4fL8K
Athari za mafuriko Mai Mahiu nchini Kenya.
Athari za mafuriko Mai Mahiu nchini Kenya.Picha: LUIS TATO/AFP

Awali afisa mmoja wa polisi katika eneo hilo, Stephen Kirui, alikuwa ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba bwawa la Kijabe lililoko katika eneo hilo la Mahi-Mahiu lilivunja kingo zake na kubeba matope, mawe na pia kung'oa miti.

Soma zaidi: Bwawa lapasua kingo Kenya, watu 45 wapoteza maisha

Lakini katika taarifa iliyotolewa jana jioni, serikali ya Kaunti ya Nakuru ilisema kuwa mafuriko hayo yalitokana na kuziba kwa njia ya reli.

Magari yalikwama kwenye tope hizo huku wahudumu wa afya wakiwatibu waliojeruhiwa wakati maji hayo ya mafuriko yakiendelea kufunika maeneo mengine.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa watu 109 wamelazwa hospitalini huku wengine 49 wakiwa hawajulikani walipo.