1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kwanini Wapakistan hawajali kuhusu uchaguzi ujao

Shamil Shams | Iddi Ssessanga
27 Desemba 2023

Je, mzozo wa kiuchumi unaoendelea na kutoaminiana kwa jumla na kutoridhika na siasa za Pakistan kunaweza kuwa sababu ya raia wa nchi hiyo kutoonyesha shauku juu ya uchaguzi ujao?

https://p.dw.com/p/4abCR
Karachi Pakistan| Soko la bidhaa la Karachi
Mfumuko wa bei wa Pakistan ulipanda hadi rekodi ya asilimia 31.4 mnamo Septemba, na watu wengi wanapambana kupata riziki.Picha: Rizwan Tabassum/AFP

Hakuna msukosuko wowote wa kabla ya uchaguzi huko Karachi, kitovu cha kifedha cha Pakistani, ingawa hivi sasa ni uhakika kwamba uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 8 hautacheleweshwa.

Kuna sababu nyingi za kutokuwa na shauku na uchaguzi mkuu ujao miongoni mwa umma; ya kwanza ikiwa ni ukandamizaji unaoendelea dhidi ya chama cha aliyekuwa waziri mkuu Imran Khan, cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI).

Khan na wasaidizi wake wengi wako jela katika kesi kadhaa, na hakuna uwezekano kwamba wataachiliwa kabla ya uchaguzi. Hatua hizi zimeifanya kura inayokuja kuwa na utata.

Pia, Pakistan imekuwa katika hali ya msukosuko wa kiuchumi kwa takriban miaka miwili. Kupanda kwa mfumuko wa bei kumewafanya raia kukosa uwezo wa kununua hata bidhaa za msingi za chakula na kulipa bili za umeme, miongoni mwa matatizo mengine. Huku wananchi wengi wakihangaika kutafuta riziki, hawasumbuki sana kuhusu nani ataunda serikali ijayo.

Masuala ya usalama ya nchi hiyo yanasalia kuwa chanzo cha wasiwasi mkubwa kwa uongozi wake wa kijeshi, huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya wanamgambo katika majimbo ya Balochistan na Khyber Pakhtunkhwa yanayopakana na Afghanistan.

Imran Khan ana kiu ya kukomesha machafuko Pakistan

Zaidi ya hayo, majenerali hao bado wanayumbayumba kutokana na maandamano ya Mei 9 ya wafuasi wa Imran Khan ambayo yalishuhudia baadhi ya waandamanaji wakishambulia majengo ya kijeshi na maeneo ya makazi.

Kutokuaminiana kati ya taasisi za serikali ni kukubwa sana kiasi kwamba uchaguzi ujao hauhusu tena ni chama gani kitashinda viti vingi katika bunge lijalo; ni kuhusu kunusurika kwa Pakistani kama taifa la kisasa, watu wengi wanasema.

Khan, mvurugaji

Uchaguzi unaokaribia wote unahusu mtu mmoja: nyota wa zamani wa kriketi aliyegeuka mwanasiasa Imran Khan. Kwa sasa anazuiliwa kwa tuhuma zinazohusiana na ufisadi na uvujaji wa siri za serikali.

Baada ya kuondolewa madarakani mwaka jana katika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni, Khan aliishutumu Marekani na baadhi ya majenerali wa kijeshi kwa kupanga njama ya kumwondoa madarakani.

Waziri Mkuu huyo wa zamani, ambaye kwa mujibu wa kura nyingi za maoni anasalia kuwa mwanasiasa maarufu zaidi nchini humo, alizidisha hatari kiasi kwamba wakati fulani mwanzoni mwa mwaka huu, taasisi za serikali zililumbana zenyewe kwa zenyewe, na baadhi ya makundi ya raia katika makabiliano ya moja kwa moja na jeshi - jambo ambalo nchi haikuwahi kushuhudia hapo awali.

Soma pia: Mahakama Pakistan yaridhia dhamaa Imran Khan

Kwa baadhi, siasa za uvurugaji za Khan ni muhimu ili kudhoofisha udhibiti wa madaraka wa majenerali; kwa wengine, ni hali ya hatari kwa nchi ambayo ina uchumi unaoelekea kuporomoka na inakabiliwa na changamoto nyingi za kijiografia.

Pakistan| Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan
Kukosekana kwa Imram Khan kwenye uchaguzi ujao nchini Pakistan kumepunguza hamasa ya raia kueleke zoezi hilo.Picha: Mohsin Raza/REUTERS

"Siasa za mgawiko za kiongozi yeyote maarufu ni hatari katika nchi yoyote kwani zinazuia utekelezaji wa mageuzi muhimu na maendeleo," Adnan Rehmat, mwandishi wa habari na mchambuzi wa Islamabad, aliiambia DW.

"Cha kusikitisha ni kwamba, Imran Khan amebobea katika siasa za chuki na matamshi ya uchochezi. Katika nchi jamii na mirengo tofauti ya kisiasa kama vile Pakistan, mgawanyiko wa kisiasa unazuia ushirikishwaji na ushirikiano unaohitajika kutatua matatizo yanayoendelea."

Rehmat ana maoni kwamba Khan amekuwa mwathirika wa "siasa zake mwenyewe za chuki," na sasa hakuna mtu anataka kutetea haki zake.

Mgogoro wa kiuchumi

Yumkini uchumi wa Pakistani ndio mwathirika mkubwa zaidi wa vurugu za muda mrefu za kisiasa. Ingawa viashiria vya kiuchumi havikuwa vyema sana wakati wa uongozi wa Khan (2018-2022), vilishindwa tangu kuondolewa kwa Khan kutoka mamlakani.

Soma pia:Nawaz Sharif arejea Pakistan baada ya miaka minne 

"Wale wenye kipato cha chini wameathiriwa zaidi na matatizo ya kiuchumi, ambapo wengi wao wamepoteza kazi na kupunguki kipato. Kwa sababu hiyo, wamelazimika kupunguza kiasi na ubora wa chakula wanachoweza kumudu, kutafuta njia za usafiri wa gharama nafuu, na kufanya kazi nyingi ili kujikimu," Jarida la Lancet lilisisitiza mwezi Septemba, na kuongeza kuwa "usimamizi mbaya wa kifedha na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, unaotokana na uingiliaji kati wa kijeshi, umezidisha mzozo wa kiuchumi."

DW imeshuhudia foleni ndefu nje ya maduka ya mikate na maduka makubwa, na watu wengi wasio na makazi wakilala kando ya barabara mjini Karachi. Mfumuko wa bei wa Pakistan ulipanda hadi rekodi ya asilimia 31.4 mwezi Septemba, ambapo bei za nishati zimekuwa juu hasa.

Baadhi ya watu hapa wana maoni kwamba ni serikali iliyochaguliwa pekee iliyopewa mamlaka na raia inayoweza kutatua matatizo haya ya kiuchumi, lakini Akhter Mohammadi, muuza chai katika eneo la Karachi katika Barabara ya Tariq, anasema nchi inahitaji kuwekwa kwenye njia sahihi kwanza.

"Bila shaka nitapiga kura (katika uchaguzi ujao). Nitampigia kura Maulana Fazal-ur-Rahman (mhubiri wa Kiislamu) kwa sababu uchumi unaweza kutatuliwa tu ikiwa Pakistan itakuwa imara kisiasa," Mohammadi aliiambia DW.

Mapango yawahifadhi wasio na makaazi Pakistan

Kurejea kwa Imran Khan?

"Hakuna kwamba PTI itashinda kwa kiasi kikubwa ikiwa uchaguzi utafanyika kwa njia ya haki. Hii ndiyo sababu wenye mamlaka wanainyima uwanja sawa.

Hata hivyo, hatimaye, si kura zilizopatikana bali viti vinavyopatikana katika bunge litakaloamua nani ataingia madarakani.

Soma pia: Chama cha Imran Khan chapata mwenyekiti mpya

Kwa maana hii, mazingira yameundwa kukifanya chama cha PTI kisifanikiwe," mchambuzi Rehmat alisisitiza.

Wataalamu wanaamini kuwa idadi ya wapiga kura itakuwa ndogo - pengine idadi ndogo zaidi katika historia ya uchaguzi nchini Pakistan.

"Jambo muhimu kwa ushiriki wa wapigakura litakuwa ikiwa wafuasi wa Khan watajitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi au la," Rehmat alisema.

Hivi sasa, hilo inaonekana kama lisilowezekana sana.