1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je viongozi wa Afrika wanatosha kusuluhisha migogoro yao?

Lilian Mtono
20 Desemba 2022

Wakuu wa zamani wa Afrika wana jukumu kubwa la kupatanisha barani Afrika, lakini wengine hawana uelewa wa mambo magumu na hwana ujuzi wa lugha jambo ambalo linadhoofisha juhudi zao za upatanishi, anansema Isaac Mugabi.

https://p.dw.com/p/4LCia
Pretoria | Waffenstillstandsabkommen für Äthiopien
Picha: PHILL MAGAKOE/AFP

Kwa zaidi ya miongo mitatu wapatanishi wa Afrika wamehusika katika kutatua migogoro ya wenyewe kwa wenyewe katika eneo la Maziwa Makuu barani humo, kuanzia Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda hadi Uganda.

Baadhi ya marais wa zamani ambao baadaye walikuja kuwa wapatanishi kama Olusegun Obasanjo wa Nigeria na Uhuru Kenyatta wa Kenya hawakuwahi kukabiliana na vuguvugu la waasi wakati wa mihula yao ya uongozi. Kwa kuwa hali iko hivyo, ni kwa kiasi gani wanaweza kutatua migogoro kwa ufanisi ambayo inaonekana kushindikana?

Mvuto.

Katika mahojiano na DW, profesa wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Wits cha Afrika Kusini Gilbert Khadiagala amesema wakuu hao wa zamani hupokelewa kwa heshima kubwa na mara nyingi wanakubalika kama wapatanishi na pande zote zinazohasimiana na hiyo huwapa nguvu ya kuingilia kati migogoro hii kwa sababu tatizo la Afrika ni kwamba mara nyingi migogoro hii inahitaji mpatanishi wa ngazi za juu sana.

Ametolea mfano Uhuru Kenyatta anayeongoza mazungumzo ya suluhu ya mzozo nchini DRC. Kenyatta aliyaambia makundi ya waasi wa kigeni yaliyoko nchini humo ama kuondoka au kukabiliana na wanajeshi wa DRC na Afrika Mashariki. Lakini waasi hao wamepuuza wito wake, na hivyo kutilia shaka uwezo wa Kenyatta katika kufikia makubaliano ya amani ya kudumu kati ya serikali ya Kinshasa na makundi kadhaa ya waasi wanaoendesha harakati zao nchini DRC.

Soma Zaidi:DRC na Rwanda zapata mwafaka kuhusu vita mashariki mwa DRC

DR Kongo Kenias ehem. Präsident Uhuru Kenyatta in Goma
Uhuru Kenyatta, mjumbe maalumu wa Afrika Mashariki kwenye usuluhishi wa mzozo wa Kongo akiwasili katika kambi ya wakimbizi iliyoko Goma.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Uwezo wa Uhuru Kenyatta.

Wakati huo huo, Khadiagala anahisi kwamba Kenyatta ni lazima atumie ujuzi wake licha ya kikwazo cha lugha ya Kifaransa ambacho mara nyingine kinamzuia katika jitihada za kupatanisha. Kenyatta ameshiriki pia mazungumzo ya usuluhishi wa mzozo kati ya Ethiopia na waasi wa Tigray nchini Afrika Kusini.

Lakini Adolph Mbeine, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Makerere, aliiambia DW kwamba anadhani Uhuru amefanya kazi nzuri katika mazingira magumu kwa sababu matatizo ya Afrika ni makubwa na magumu.

Udhaifu wa Uhuru Kenyatta.

Frederick Golooba-Mutebi, mchambuzi wa kujitegemea aliyebobe katika masuala ya eneo la Maziwa Makuu, anasema rais Kenyatta hajakutana na waasi wa M23 wanaolaumiwa kwa machafuko mashariki mwa Kongo. Golooba anaamini kwamba Kenyatta anaongoza "mazungumzo ya uwongo" kwa sababu alialika makundi yanayotuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu na yaliyoshirikiana na serikali huko Kinshasa na si M23.

Kombibild Felix Tshisekedi und Paul Kagame
Kumekuwa na mabadilishano ya lawama baina ya rais Felix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda kuhusiana na mashambulizi ya waasi wa M23 nchini Kongo.

Amesema anadhani upatanishi nchini Kongo unashindikana kwa sababu watu wanaojaribu kusuluhisha hawana ufahamu wa kutosha, lakini pia kukosekana kwa wahusika wawili muhimu na wenye uelewa wa kutosha kuhusu mgogoro huo na ambao anadhani wanafaa kulisuluhisha, ambao ni rais wa Rwanda Paul Kagame na Yoweri Museveni wa Uganda.

Urafiki wa Kagame na Uhuru

Uwezo wa Kenyatta kukamilisha kazi yake upatanishi umekuwa ukihojiwa kwa sababu ya ukaribu wake na rais Paul Kagame. Profesa Khadiagala anasisitiza kwamba Uhuru tayari amehujumiwa kutokana na uhusiano wake na Kagame na huenda ikawa vigumu kwake kujiondoa. Kwake yeye upatanishi unaanzia kwenye msingi mgumu sana kwa sababu kuna muhusika kama Kagame ambaye serikali yake imeshutumiwa kuwaunga mkono M23, lakini akitaka kuonekana kama asiyeegemea upande wowote.

Wasuluhishi wanaweza kuwa na upande?

Kujenga uaminifu kati ya wapatanishi na pande zinazozana ni muhimu ili kukomesha uhasama. Kwa mfano, chama cha TPLF cha Tigray kilimwona rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo kuwa yuko karibu na serikali ya Ethiopia na waziri mkuu wake Abiy Ahmed wakati wa mazungumzo ya kumaliza mapigano katika eneo la Tigray.

Umoja wa Afrika ulimpa kazi Obasanjo ya kuwa mpatanishi kati ya serikali na TPLF. Lakini kulingana na Phil Clark kutoka SOAS, Obasanjo anaonekana kuwa na upendeleo na hajaweza kuwashawishi wanamgambo hao kama ni mtu wa katikati. Kulingana na Clark, wahusika wengi wa mizozo mara nyingi huhoji ikiwa wapatanishi waliwahi kukabiliana na harakati za waasi katika serikali zao, huku wachambuzi wengi wakiamini kwamba mara nyingine hakuna ulazima wa wapatanishi wakati pande zinazopigana ziko tayari kuzungumza.