1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel, Hizbullah washambuliana tena

Mohammed Khelef
8 Januari 2024

Jeshi la Israel limeshambulia kwa mara nyengine maeneo kadhaa nchini Lebanon, huku Hizbullah ikiharibu kituo cha kuongozea ndege kaskazini mwa Israel na wasiwasi ukiongezeka juu ya uwezekano wa vita kamili baina yao.

https://p.dw.com/p/4ayDM
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya Israel kwenye eneo la kusini mwa Lebanon.
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya Israel kwenye eneo la kusini mwa Lebanon.Picha: Ramiz Dallah/Anadolu/picture alliance

Jeshi la Israel lilisema asubuhi ya Jumatatu (Januari 8) lillishambulia kituo cha kijeshi cha kundi la Hizbullah karibu na mji wa Marwahin kusini mwa Lebanon na kituo chengine cha kurushia makombora katika eneo la mpakani. 

Jeshi hilo liliongeza kwamba droni na helikopta yake zilishambulia pia maeneo ambayo yalitumika kuishambulia Israel. 

Kundi la Hizbullah, ambalo lina mafungamano na Hamas na Iran, limekuwa kwenye makabiliano ya hapa na pale na Israel katika siku za hivi karibuni. 

Soma zaidi: Borell aonya Lebanon kuingizwa vitani Mashariki ya Kati

Kwa mujibu wa jeshi la Israel, makombora yaliyorushwa na Hizbullah hapo jana yalikiharibu kituo cha kuongozea ndege kwenye Mlima Meron ingawa hakikuharibu mifumo yake ya ulinzi wa anga, wala kuuwa mwanajeshi wake yeyote. 

Hizbullah iliyaelezea mashambulizi hayo kuwa ni "jibu la awali" kwa mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya kiongozi wa ngazi wa juu wa Hamas kwenye ngome ya Hizbullah mjini Beirut wiki iliyopita. 

Mkuu wa jeshi la Israel, Luteni Kanali Herzi Halevi, alisema shinikizo dhidi ya Hizbullah kuingia kwenye vita linaongezeka, na kuna uwezekano wa pande hizo mbili kuingia kwenye vita vya moja kwa moja. 

Marekani, Ujerumani zapigania mzozo usitanuke

Hofu hiyo ya kutanuka kwa vita vya Gaza ndiyo iliyowafanya mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Ujerumani kufanya ziara kwenye eneo la Mashariki ya Kati muda huu. 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Baerbock.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Baerbock.Picha: Annette Riedl/dpa/picture alliance

Annalena Bearbock anapanga kuutembea Ukingo wa Magharibi hivi leo kukutana na mwenzake wa Palestina, Riyadh al-Maliki mjini Ramallah. Kesho atakwenda nchini Lebanon kukutana na viongozi wa huko. 

Soma zaidi: Baerbock kufanya ziara Mashariki ya Kati siku ya Jumapili

Kwa upande wake, Antony Blinken amekutana na kiongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan, na anapanga kukutana na Mwana Mfalme wa Saudi Arabia Mohammad bin Salman kabla ya kuitembelea Israel hivi leo katika kile anachosema ni jitihada za kuzuwia mgogoro huo kutanuka zaidi. 

Akiwa mjini Doha, Qatar, Blinken amewaambia waandishi wa habari na hapa namnukuu: "Mgogoro huu unaweza kutanuka ukawa mkubwa kabisa na kusababisha ukosefu mkubwa zaidi wa usalama na majanga zaidi." Mwisho wa kumnukuu.

Kwenyewe Gaza, idadi ya Wapalestina waliokwishauawa hadi sasa imefikia 22,800 huku 58,000 wakijeruhiwa tangu kuanza kwa vita, kwa mujibu wa wizara ya afya ya ukanda huo unaodhibitiwa na Hamas.

Maafisa wa afya wanasema asilimia 70 ya waliouawa na majeruhi ni wanawake na watoto.

Vyanzo: Reuters, DPA, AP