1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo kutokana na mafuriko Kenya yaongezeka hadi 228

6 Mei 2024

Idadi ya vifo vilivyosababishwa na mafuriko imefikia 228 na wengine 200,000 wameathirika.

https://p.dw.com/p/4fXqy

Wakati huouo, shughuli ya kubomoa nyumba zilizoko pembezoni mwa mito na kwenye njia ya maji inaendelea jijini Nairobi.

Kwa upande mwengine, hofu ya mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza yanayosambazwa na maji imezuka baada ya vyoo na mabomba ya maji taka kuharibika.

Katika kaunti ya Tana River, takriban watu 30 wanaripotiwa kuambukizwa kipindupindu baada ya mto Tana kufurika. Wizara ya afya imeahidi kuwasaidia wakaazi kwa nyenzo na kuhamia maeneo salama.

Msaada wa vyandarua na dawa kwa wakaazi

Akiwa ziarani siku ya Jumapili kwenye bonde la Tana, katibu katika wizara ya afya Mary Muthoni alibainisha kuwa serikali kuu itafanya lililo ndani ya uwezo wake kuzuwia maambukizi ya kipindupindu kusambaa. Kadhalika ameahidi kuwa wiara hiyohiyo inajiandaa kugawa vyandarua vya mbu pamoja na vidonge vya lishe, dawa na vifaa vya maabara ili kuepusha mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza yanayosambazwa na maji na pia malaria. Mvua inaendelea kunyesha kote nchini.

Bwawa lapasua kingo na kusababisha maafa Kenya

Soma pia: Ruto aahidi kuhamishwa wananchi ambao wamekubwa na mafuriko

Shughuli ya kubomoa nyumba zilizoko pembezoni mwa mto Nairobi inaendelea. Hali ni mbaya mtaani wa Mukuru wa Reuben. Mabati yaliyochakaa yametupwa kila mahali na wakazi wanajitahidi kuokoa mali  zao ili kujaribu kuanza maisha mapya kwenye sehemu wasiyoijua.

Joshua Masese ni mkaazi wa Mukuru na anahisi wameachwa katika hali mbaya kwani,” Wakianza kubomoa nyumba sharti watupe notisi ndio tujipange ili vitu ulivyonunua ndio uviokoe. Huwezi kutoroka uviache vitu vyako.”anasimulia.

Wakaazi kuhama maeneo yaliyo karibu na mto

Mtaani Kiambiu, Nancy Murangeti alijifungua wiki moja iliyopita na alilazimika kuhamia nyumba nyengine baada ya ile aliyokuwamo kuharibiwa na maji. Anayoishi kwa sasa haina tofauti kubwa ila angalau yeye na wanawe 5 wanapata stara lakini,Hii nyumba ninamoishi inavuja. Hata huko juu kwenye kitanda tumeondoa godoro kwa kuwa linatota.Imebomoka pale pembeni na mvua inaingia ndani.Mvua ikiendelea ukuta unakuwa na shimo.” anafafanua. 

Mafuriko yaua watu 10 jijini Nairobi Kenya

Soma pia: Mafuriko yakwamisha watalii karibu 100 Maasai Mara

Kwa mujibu wa wizara ya usalama wa taifa,idadi ya vifo imefikia 228 na watu laki 227 wameathiriwa na mafuriko tangu mvua kuanza kunyesha mwezi wa Machi mwaka huu kote nchini. Ili kuepusha madhara zaidi ,serikali imewaamuru wakaazi wa mitaa iliyo pembezoni mwa mto kuhama.

Mwanaisha Chidzuga ni naibu msemaji wa serikali ya Kenya na aliutembelea mtaa wa Mukuru ambako alisisitiza kuwa,”Sio muda kidogo tuliowapa ni kutokana na hali ilivyo. Kama munavyoona tayari mvua inaendelea kukusanyika….na kunyesha. Tungependa tuwapatie muda zaidi lakini wanasema tahadhari kabla ya hatari.”anaelezea.

Mto Nyando umefurika na kuvunja kingo

Serikali imeahidi kuwashika mkono wakaazi wa maeneo ambayo wanapaswa kuyahama. Kaunti 33 kati ya zote 47 zimeathiriwa na mvua nyingi inayoendelea kunyesha iliyosababisha mabwawa kujaa pomoni na mito kuvunja kingo zake. Mto Nyando ulioko kaunti ya Kisumu ulivunja kingo zake wikendi iliyopita na wakaazi wanahitaji usaidizi wa kuondoka na pia pahala pa kujistiri.

Ludia Achieng ni mfanyabiashara eneo la Ahero huko kaunti ya Kisumu anakouza ndizi na maji ya mto Nyando uliofurika yamemuathiri kwani,Maji yalikuja mengi yakanishtua. Ndizi zangu zote zilienda na maji. Sina chochote,hakuna kilichosalimika. Hata sijui nitarejea vipi kwetu Kabondo huko Homabay.”amelalamika. 

Yote hayo yakiendelea,mipango inaendelea ya kufanya ibada ya pamoja kwaajili ya waliopoteza maisha yao kwenye mkasa wa Mai Mahiu pale handaki la zamani la relini lilipojaa maji na kumimina tope kijijini Kamachuru huko Kijabe. Watu 58 waliuawa, 52 walijeruhiwa na wengine 52 bado hawajulikani waliko. Kwa upande wake, idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya inatahadharisha kuwa mvua bado iko njiani ijapokuwa vipindi vya jua vinaendelea kushuhudiwa.

Kadhalika, bunge la taifa linasubiriwa kutoa ridhaa ya shilingi bilioni 10.6 kwa matumizi ya dharura ya wahanga wa mafuriko.

Msalaba Mwekundu waongoza juhudi za uokoaji mafuriko Kenya