1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kimya kuhusu migogoro ya kisiasa Afrika Magharibi

12 Novemba 2020

Uchaguzi uliopingwa Cote d'Ivoire na Guinea, vurugu Nigeria, Waafrika Magharibi wanatumai kupata msaada wa kigeni, lakini Umoja wa Ulaya umejiweka kando. Haujachukua hatua yoyote ya wazi

https://p.dw.com/p/3lAjt
Elfenbeinküste I Straßenansicht in Toumodi
Picha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

Rais wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara hakupaswa kuwa kwenye karatasi za kura. Lakini kiongozi huyo aliyekuwa tayari amekamilisha mihula miwili alitaka wa tatu madarakani, na kupitia mwanya wa kisheria, Ouattara akagombea. Licha ya hasira ya upinzani na kutishia Amani nchini Cote d'Ivoire akashinda kwa asilimia 94 ya kura, uliosusiwa na upinzani. 

Soma pia: Ouattara ashinda muhula wa tatu Cote d'Ivoire kwa kishindo

Mgogoro wa kisiasa Cote d'Ivoire bado haujakwisha. Upinzani umekataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi, na maandamano yenye vurugu tayari yamesababisha vifo.

Umoja wa Ulaya haujachukua hatua. Jumuiya hiyo yenye nguvu ilisema imeyazingatia matokeo, kwa mujibu wa mkuu wa sera za kigeni Joseph Borrel. Borrel alisema umoja huo unatarajia pande zote zilizohusika zichangie katika kutuliza hali na kurejea kwenye mazungumzo.

Brüssel | Pressekonferenz zur EU-Afrika-Strategie mit Josep Borrell
Umoja wa Ulaya haujakemea wizi wa kura na ukatili dhidi ya raia Afrika MagharibiPicha: picture-alliance/Zuma/N. Landemard

Maneno ya kuonya, lakini hakuna hatua

Katika mwaka huu wa 2020, Rais wa Guinea mwenye umri wa miaka 83, Alpha Conde, aliibadilisha katiba ya nchi, akagombea katika uchaguzi na akashinda. Na kama tu Cote d'Ivoire, machafuko yalizuka na tuhuma za udandanyifu wa kura zikatolewa. Lakini Umoja wa Ulaya ulikuwa na maneno tu ya kiuonya nchi hata ingawa uadilifu wa uchaguzi huo ulitiliwa shaka.

Matukio nchini Nigeria yameshughulikiwa vivyo hivyo. Serikali inakabiliwa na shinikizo wakati vijana wakiongoza maandamano dhidi ya ukandamizaji, machafuko ya polisi na ufisadi serikalini. Polisi wamejibu kwa kutumia nguvu kupita kiasi, na kusababisha vifo vya watu 12 mpaka sasa. Na bado, Umoja wa Ulaya umesalia kimya.

Guinea Präsidentschaftswahlen | Alpha Conde
Conde aliwahia muhula wa tatu baada ya kuibadili katibaPicha: John Wessels/AFP

Soma pia:Wawakilishi wa UN na ECOWAS wawasili Guinea kutuliza vurugu

Brussels inapendelea suluhisho la kikanda

Watu wengi katika nchi zilizoathirika za Afrika Magharibi wamefadhaishwa na kimya cha Umoja wa Ulaya.  Ramadan Diallo, msomi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Sonfonia-Conakry nchini Guinea anasema hali hiyo inaonyesha kuwa jamii ya kimataifa haitaki kujihusisha Zaidi ya kiwango Fulani. Diallo ameiambia DW kuwa itabidi Afrika Magharibi itumie raslimali za kikanda kuyatatua matatizo yake. Kwa sababu nchi hizi haziwezi kutegemea chochote kutoka jamii ya kimataifa.

Robert Kappel, msomi anayebobea katika uchumi na siasa za Afrika, anapinga hilo akisema Umoja wa Ulaya hujihusisha na mizozo ya Afrika. Anataja miradi ya mafunzo kwa majeshi ya kikanda nchini Mali. Anasema Umoja wa Ulaya pia unaunga mkono jeshi hilo kwa matumaini ya kuwatokomeza wanamgambo wa itikadi katika katika eneo la Sahel.

Soma pia: Rais wa Nigeria aacha mauwaji ya watu 12 nje ya hotuba yake

Kwa mujibu wa Kappel, Umoja wa Ulaya unajiepusha na uchaguzi huo uliopingwa nchini Cote d'Ivoire kwa sababu rahisi. "Umoja wa Ulaya unazitegemea mamlaka za kikanda kama Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi – ECOWAS kuutatua mgogoro huo.”

ECOWAS imeingilia kati mizozo mingi ya kisiasa Afrika Magharibi, kama vile nchini Mali 2013 na Gambia 2017. Kappel anasema Umoja wa Ulaya kuingilia kati Afrika sio tena hatua yenye tija. Kwa mfano baadhi ya serikali za Afrika zinaiona Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuwa chombo cha kuyalinda maslahi ya nchi za Magharibi na Ulaya barani humo.

EU inashughulika nyuma ya pazia?

Mali Bundeswehr EU-Ausbildungsmission EUTM
Jeshi la Ujerumani limekuwa likiwapa mafunzo askari wa MaliPicha: Imago Images/photothek/T. Wiegold

Mwakilishi wa Wakfu wa Ujerumani wa Friedrich Ebert nchini Cote d'Ivoire Thilo Schöne anayejihusisha na chama cha Social Democratic anasema nyuma ya pazia, ni habari nyingine.

Soma pia: Ufaransa na nchi za Sahel kutathmini vita dhidi ya makundi ya kigaidi

Anasema Umoja wa Ulaya ni mmoja wa waongozaji wa juhudi za upatanishi kati ya serikali na upinzani akiongeza kuwa mabalozi kutoka mataifa kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakifanya mazungumzo na serikali ya Cote d'Ivoire.

Umoja wa Ulaya unataka kujiweka kando katika migogoro ya ndani ili kueouka kuegemea upande mmoja kama madola ya magharibi. Halmashauri Kuu ya Ulaya ilizindua mkakati mpya kwa Afrika. Unasisitiza Zaidi katika kuzisaidia taasisi za Kiafrika, jeshi na mashirika ya kijamii. Hii ni tofauti na mkakati wa uingiliaji wa kijeshi ambao umeonekana kutofua dafu katika miaka kadhaa iliyopita.

Bruce Amani
Makala hii ilichapishwa kwanza katika DW Kijerumani